Vyombo vya Usalama, Wafanyabiashara, Watajwa Mtandao wa Madawa ya Kulevya Nchini

Jeshi
la Wananchi, Polisi, Uhamiaji na vyombo vingine vya usalama pamoja na
baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara maarufu nchini wametajwa
kujihusisha na biashara haramu ya madawa kulevya ambayo imeharibu maisha
ya maelfu ya vijana na kuvunja vunja familia. Taarifa za kuhusika huku
kwa maafisa wa vyombo hivi vya usalama na watu hawa mashuhuri zimekuja
baada ya mmoja wa vijana wa Kitanzania aliyekamatwa huko Hong Kong
kuandika barua ya kukiri kuhusika kwake na bishara hiyo pamoja na
kuwataja watu waliomuingiza na kumwezesha kufanya biashara hiyo.
Barua
hiyo ilipostiwa katika mojawapo ya tovuti zinazofuatilia mambo ya
madawa ya kulevya na kubandikwa chini ya kichwa cha habari cha “Punda wa
Madawa” kwenye mtandao wa waumini wa Kanisa Katoliki ambao umeundwa ili
kuunga mkono mabadiliko na mafundisho ya Mtaguso wa Pili wa Vatikano.
“Punda wa Madawa” ni jina linaloelezea watu wale wanaotumiwa na kutumika kusafirisha madawa
ya kulevya kutoka kwa wafanyabiashara wa jumla kwenda kwa
wafanyabiashara wa reja reja. Watu hawa wanaweza kuwa ndani ya nchi au
kati ya nchi na nchi. Mara nyingi – kama jina linavyoashiria – watu hawa
ni vyombo tu vya vinara wa madawa wa kulevya na lolote litakalowakuta
huwa ni juu yao wenyewe. Hata hivyo, endapo wanafanikiwa kusafirisha
‘mzigo’ kutoka pointi moja kwenda nyingine basi huweza kulipwa vizuri na
wengine huishi maisha ya kifahari kabisa kutokana na biashara hii.
Kabla
ya kwenda kuwataja watu ambao mwandishi anawatuhumu kujihusisha na
biashara hii mtunzi wa barua hii anaelezea kwa kirefu jinsi alivyoingia
katika mtego wa kujihusisha na biashara hiyo na hatimaye kujikuta
akiangukia kwenye mikono mikali ya sheria ya polisi wa Hong Kong, China.
Mwandishi anaelezea kwa kirefu kuwa aliingia katika biashara hiyo baada
ya shida za maisha kumzidia na kujikuta hana njia ya kupata kipato
kingine halali ili kuisaidia familia yake na hivyo kuamua kutumia njia
za mkato.
“Pamoja na misukosuko yote hiyo nilivumilia,
lakini mtihani mkubwa ni pale kodi ya nyumba ilipoisha na mwenye nyumba
akanipa notice ya mwezi mmoja (nihame), au nimpe kodi ya miezi ya
360,000tsh” ameelezea mwandishi huyo ambaye hakuweka jina lake.
Mwandishi huyo wa barua anadai kuwa baada ya kujitahidi kutafuta fedha
hiyo na kushindwa alijikuta ameomba msaada kwa marafiki zake ambao
anawaita ‘wabaya’ kwani ni wao ndio walimchukua na kumpeleka kwa bosi
wao ambaye alimlipia kodi ya miezi sita na kumpa fedha za ziada za
shilingi laki mbili. Tajiri huyo ni mtu anayeishi Magomeni Mwembechai.
Ni
hapo ndipo alipoanza kupewa mazoezi ya kumeza vidonge vya heroin. Siku
chache baadaye alijikuwa amepewa vidonge 93 vya madawa hayo ambavyo kila
kimoja kina gram 15 kwa jumla ya gram 1395 (sawa na paundi tatu
hivi-MM). Kutokana na kuanza kupata matatizo na kutoka vidonda kijana
huyo alijaribu kutaka kuacha biashara lakini akakumbushwa kuwa ana deni
la 560,000Tsh na upande mwingine aliahidiwa kuwa endapo angefikisha
mzigo ule salama basi angelipwa dola 5000. Akapewa mpango wa safari
kwenda Hong Kong akiwa katika hali ya udhaifu mkubwa wa mwili.
Mwandishi
alitarajia kuwa kutokana na hali mbaya basi wangekamatwa uwanja wa
ndege wa Mwalimu Nyerere jijini Dar. Hiyo haikuwa hivyo kwani kwa
maelezo yake “Ajabu pale airport kulikuwa na mtu ambaye aliandaliwa
kunipitisha mimi mpaka boarding room” anasema kijana huyo. Ilikuwa ni
hali aliyokuwa nayo ndiyo iliwafanya maafisa wa Hong Kong kumtilia shaka
na kumweka kizuizini.
Kitu ambacho mwandishi
inaonekana hakuwa anakijua ni kuwa Hong Kong hawana huruma na watu
wanaojihusisha na madawa ya kulevya kwani wana vifungo vikali kabisa na
kwa maelezo yake kuwa hadi hivi sasa kuna vijana wa Kitanzania karibu
150 ambao wameshafungwa na wengine wakiendelea kusubiri kesi zao
ziendelee. Alichoshukuru Mwandishi ni kuwa angalau yeye na wenzake
wamekamatwa Hong Kong kwani kama wangekamatwa China yenyewe basi
wangenyongwa kwani tayari – kwa maelezo yake – wapo vijana wa Kitanzania
walionyongwa huko.
Kwa maelezo yake ambayo
yanashabihiana kwa kiasi kikubwa na taarifa za vyombo vya usalama vya
kimataifa vinavyofuatilia biashara hii haramu mizigo ya madawa ya
kulevya yanaingia nchini Tanzania yakitokea Pakistani na Afghanistan
kupitia maeneo ya Tanga, Dar, Mtwara na Bagamoyo ambayo huja kwa boti na
kupokelewa na wahusika wakubwa nchini.
Ikumbukwe
kuwa mwaja jana Januari mtoto wa aliyekuwa afisa wa Benki Kuu Amatus
Liyumba aitwaye Morine alikamatwa na wenzake huko Lindi akiwa na mzigo
wa madawa ya kulevya wenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 9!
“Mizigo
hiyo huwa inasindikizwa na magari ya jeshi na polisi na hii siyo siri
kwani hata wahusika wanajua” amesema kijana huyo katika barua hiyo
ambayo imewashtua Watanzania wengi baada ya kupostiwa katika mtandao
maarufu wa JamiiForums siku ya Jumamosi.
Kuhusishwa
kwa vyombo vya usalama na biashara hii haramu si jambo la kushangaza
kwa watu ambao wamekuwa wakifuatilia kuenea kwa vitendo vya uhalifu
nchini. Ipo mifano kadha wa kadha ambayo inaonesha kuwa baadhi ya
watumishi wa vyombo hivi vya usalama wako ‘compromised’ na haijulikani
ni nani anaweza kuaminika. Baadhi ya mifano ni hii ifuatayo:
- · Mwaka 2011 – Mwanajeshi wa JWTZ alikamatwa mjini Morogoro akijaribu kusafirisha magunia 12 ya bangi kutoka Iringa kuja Dar. Hii ilikuwa ni mwezi Disemba mwaka huo. Kijana huyo wa miaka 26 alikamatwa na askari wa polisi waliokuwa doria akiwa amevaa sare za jeshi hilo. Ni afisa wa Kambi ya Lugalo mwenye namba MT86879.
- · Januari 2013 – Afisa wa JWTZ mwenye namba MT 59503 Sajenti Aziz Athumani alikamatwa huko Arusha akiwa na pembe mbili za ndovu.
- · Julai 2013 – Hivi majuzi tu mwanajeshi mwingine Seleman Chasama (50) –katika hali ya kushangaza akili kabisa – amefikishwa mahakamani akishtakiwa makosa ya uhujumu uchumi na yale ya Uhifadhi wa Wanyama Pori baada ya kukutwa na pembe 357 za ndovu zenye thamani ya dola milioni 2.6.
- · Julai 2013 – kabla hilo la mapema Julai halijatulia wiki iliyopita taarifa za maafisa waandamizi wa Jeshi la Magereza kukamatwa na nyara za serikali nalo zimeonesha kuwa hata Magereza nako si salama. Maafisa hao akiwemo Mrakibu Msaidizi wa Magereza (ASP) Joseph Sauli, Warden Richard Barick na Koplo Silvester Bukha walikutwa wakitumia gari la Magereza kubeba Twiga 2, Pundamilia 2, Swalapalapala 2 na Mbuni 2 wote wakiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 55!
Hiyo
ni mifano michache tu ya kuhusishwa kwa maafisa wa usalama na mambo ya
ujangili, madawa ya kulevya na hapo hatujaangalia uhalifu mwingine. Na
hapa izingatiwe hawa ni wale ambao walikamatwa tu na hatujaangalia wale
wa polisi ambao kama watu wanakumbuka waliwahi kutuhumiwa kujaribu
kumtegeshea mtoto wa Mzee Mengi madawa ya kulevya pale Uwanja wa Ndege
na barua hii inatupa mawazo tu jinsi gani hilo linaweza kutokea kweli.
Ikumbukwe
barua hii imekuja tayari kukiwa na habari za mabinti wawili wa
Kitanzania wamekamatwa Afrika ya Kusini baada ya kutua nchini humo na
mzigo wa madawa ya kulevya wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 6;
na hawa waliondokea uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere jijini
Dar-es-Salaam. Bila ya shaka kuna kuhusika kwa maafisa wa kikosi cha
uhamiaji ambao wanawajibu wa kusimamia watu wanaoingia na kutoka nchini.
Vilevile,
barua hii imekuja siku chache tu toka Mbunge wa Musoma Mjini Vicent
Nyerere (CHADEMA) kuzungumza na waandishi wa habari kutaka serikali
ijisafishe kwani inaonekana kuwaogopa vinara wa madawa ya kulevya.
Katika tamko lake la Julai 19 Bw. Nyerere ambaye pia ni Waziri Kivuli wa
Mambo ya Ndani alisema kwa ukali kuwa “Kupuuzia na kutochukua hatua kwa
wahusika wa dawa za kulevya ni kuangamiza nguvu kazi ya taifa. Nguvu
kazi ya taifa ikishaharibiwa na dawa za kulevya hatuna taifa tena. Hivyo
Serikali ifahamu kwamba kuendelea kulifumbia macho jambo hili kwa
manufaa ya mafisadi wachache ni kulihujumu taifa na huo ni usaliti dhidi
ya kiapo ilichokula cha kulitumikia taifa na kusimamia usitawi wa
wananchi wa Tanzania. Aidha, Serikali itambue pia kwamba kuendelea kukaa
kimya bila kuchukua hatua yoyote juu ya jambo hili kunatoa dalili
kwamba yamkini ya yenyewe inahusika na biashara hiyo.”
Katika
kuhitimisha barua yake, mwandishi wa barua hiyo alienda na kuwataja
baadhi ya watu ambao wanahusika na mtandao wa madawa ya kulevya na namna
ya ushiriki wao huku akisema kuwa wapo wengine ambao majina yao
yakitajwa nchi itashtuka kwani ni watendaji wa ngazi za juu serikalini. Kwa mujibu wa kijana huyo wanaodaiwa kuhusika na biashara hiyo nchini ni hawa wafuatao (kama alivyoandika):
- 1. Beka Rangers – Yupo Magomeni Mapima na ana Bureau De Change, Magomeni.
- 2. Yasin – Yupo Sinza Madukani na amepanga floor nzima ya gofoa lililopo hapo madukani. Ana semitrailer za kusafirishia mizigo. Anajulikana sana.
- 3. Chonji – Yupo Magomeni Mwembechai na ana ghorofa analijenga hapo Mwembechai la ghorofa tano. Naye ni maarufu sana.
- 4. Ahmed Horohoro – Maarufu hapo Magomeoni Mapipa
- 5. Gatuso – Maarufu Magomeni Mapipa – Chipolopolo
- 6. Manganja – Sinza Uzuri Darajani. Ukitokea Magomeni kwenda Sinza –Uzuri baada tu ya kumaliza daraja, nyumba ya pili kushoto ndipo kuna ofisi yake.
- 7. Gasper – Vijana Kinondoni; ana ofisi ya stationery hapo vijana ni maarufu sana.
- 8. David Kanyau – Anajulikana hata na maaskari wengi.
- 9. Kogoko – Yupo Dar-es-Salaam, mizigo mingi inayoenda China ni ya kwake; maaskari wanamjua sana.
- 10. Mhe. Iddi Azzan – Magomeni – Huyu ni mbunge na asichanganywe na Musa Azzan “Zungu”.
- 11. Tanaruza – Mwembechai
- 12. Shikuba – tajiri mkubwa, serikali inamtambua.
- 13. Wanaopokea mizigo huko China ni watu aliowataja kwa majina ya Omary na Shakur.
Barua
yake hiyo ilitumwa kwa vyombo mbalimbali vya habari vya Tanzania. Kitu
kimoja ambako kiko wazi ni kuwa kijana huyo amefanya kile ambacho watu
wengi wameshindwa kukifanya japo wakiwa na uwezo wa kukifanya.
Kukithiri
kwa biashara ya madawa ya kulevya nchini kunafichua tu ya kile
kinachoendelea na kusukuma ‘gurudumu la maendeleo’ nchini ambapo wakati
watu wengine wanahenyeka kila siku kufanya kazi halali na kwa jasho lao
lipo kundi ambalo limejikita hadi kwenye madaraka ambalo licha ya
kufanya vitendo vya ufisadi serikalini lipo pia kwenye mtandao wa
uhalifu (organized crime) na limejipenyeza hadi kwenye vyombo vya dola.
Barua ya kijana huyu kuhusisha vyombo vya usalama yaweza kuwa ni andiko
la mwisho kwa serikali ya Kikwete kuangalia utendaji wa vyombo vyake
ambavyo anaonesha kuwa anaviamini sana.
Jambo la kutisha ni kuwa kutokana na watu wa makundi mbalimbali kuhusishwa na biashara
ya madawa ya kulevya tusije kushangaa hakuna mtu yeyote ambaye tunaweza
kumwamini tena. Je, serikali itapokeaje taarifa hii? Je, kuna mtu
mwenye ujasiri wa kupambana na kuufumua mtandao huu? Je, kama kijana
huyu kawafanyia kazi yote na kuwatajia majina na mahali je serikali ya
Tanzania ina maana kuwa miaka yote hii haijui watu hawa na kama haiwajui
vyombo vya usalama kwanini vinatumia “intelijigensia” nyingi kwenye
mikutano ya CDM badala ya wahalifu hawa wakubwa? Na kama watu hawa
waliotajwa hawajulikani na vyombo vya usalama au wanajulikana lakini
hawakamatwi je Kikwete anahalalisha vipi kuendelea kuwatumia watu wale
wale walioshindwa kusimamia usalama wan chi? Si ni yeye aliyesema jusi
kwenye sikukuu ya mashujaa kuwa nchi iko “salama”. Kama yaliyomo kwenye
barua hiyo ni kweli je tunaweza kusema kweli nchi iko “salama”? Salama
kwa nani?
Swali la kujiuliza na
kufikirisha: Kwa kila madawa yanayokamatwa na kwa kila watuhumiwa
wanaokamatwa ni wangapi wanafanikiwa kupita na kuishia mitaani au nchi
jirani?
CHANZO http://www.mwanakijiji.com
No comments:
Post a Comment