Wednesday, February 27, 2013

MWANAFUNZI MBEYA ANASWA NA MTANDAO WA WIZI

 


POLISI wilayani Rungwe, mkoani Mbeya, limewanasa watu wanne akiwamo mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne mwaka jana, wilayani Bunda, mkoani Mara, baada ya kukutwa wakiiba fedha Benki ya NMB tawi la Tukuyu kupitia mashine za kutolea fedha (ATM).
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Chrispin Meela alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 2:30 usiku.
Meela aliwataja watuhumiwa  hao kuwa ni mkazi wa mjini Tukuyu,  Mfanyabishara wa Mbozi, mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne mwaka jana wilayani Bunda na mkazi wa Msasani Tukuyu.
Alisema akiwa nyumbani kwake usiku, alipigiwa simu na msamaria mwema na kuambiwa taarifa za kuwapo watu  wakiwa kwenye mashine hizo za kutolea fedha, huku wakiwa wanatoa fedha mfululizo na aliwatilia shaka.
“Jana  usiku saa 2:30 nilipigiwa simu na msamaria mwema na kuniambia kuwa,  kuna watu wapo Benki ya NMB wanatoa fedha ATM tena mfululilo huko wakiwa na kadi nyingi za ATM,” alisema Meela na kuongeza:“Baada ya kuambiwa hivyo nilimpigia simu OCD (Mkuu wa polisi wilaya), akatuma timu ya makachero eneo ta tukio na wakabahatika kuwakuta na kuwatia nguvuni.”
Meela alisema watuhumiwa  walikutwa wakiwa na kadi bandia za ATM 150 za watu tofautitofauti  na kwamba, hadi wanatiwa mbaroni tayari walikuwa na Sh20.5 milioni mkononi. Alisema kadi zote ni za NMB na kwamba, zilikuwa zinaonyesha  wateja wote ni walimu kutoka wilayani Mbozi.
Alisema baada ya watuhumiwa kuhojiwa  walidai ni wafanyabiashara wanajihusisha na kukopesha fedha walimu, hivyo  katika kuzirejea fedha hizo walimu waliwapatia kadi zao ili waende kutoa  benki.
“Kinachotupa hofu  hapa ni kwamba, kadi zote hizi zinaonyesha wateja kutoka wilayani Mbozi, sasa swali kwa nini waje kutolea fedha hizo wilayani kwetu?” alihoji Meela.
Alisema watuhumiwa wote wapo Kituo cha Polisi Tukuyu kwa mahojiano zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani alikiri kupata taarifa hizo, lakini alikataa  kulitolea ufafanuzi kwa sababu  wanaendelea na uchunguzi.

No comments:

Post a Comment