Monday, March 18, 2013

Sitta: Zikataeni fedha chafu kanisani





waziri wa ushirikiano wakimataifa samweli sitta





YWaziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amewataka viongozi wa dini kuwakemea wanasiasa wanaomwaga fedha chafu kanisani kwa lengo la kutaka kuungwa mkono na waumini.
Pia amewataka viongozi hao kuzikataa fedha hizo alizodai zinapatikana kwa rushwa na wizi wa mali ya umma.
Sitta alisema hayo jana wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Bethania lililopo Tegeta jijini Dar es Salaam.
“Baba Askofu nawaomba viongozi wa kanisa msaidie sana kuondoa unafiki huu ambao sasa unaletwa kanisani,” Waziri Sitta alimweleza Askofu Mkuu wa KKKT, Dk Alex Malasusa.
Alisema,  “wapo watu wenye fedha chafu wanazileta kanisani, ninyi mnazipokea. Ni hatari sana hii, mtu anasimama madhabahuni anaanza kuwadanganya wakristo.”
Alisema wapo watu wanadanganya kwamba wao ni maskini na kwamba fedha wanazozitoa kanisani wamechangiwa na marafiki zao wakati kila mtu anafahamu kwamba ni uongo.
Aliongeza: “Wakristo tunashangilia, wakati hata ukimuita mjukuu wako na kumuuliza eti huyu ni maskini, atakueleza kuwa ni tajiri wa kukufuru,” alisema Sitta.
Alisema yeye hataacha kusema ukweli kwa sababu kuacha kufanya hivyo ni kuiua nchi hii.
“Tukiacha kuyasema haya ni kuiua nchi, sisi viongozi tukiendelea kuiibia nchi hii na vijana wanaona haya yanaendelea basi nao wataona hii ndiyo jadi nao wataiba,” alisema.
“Chonde chonde Wakristo tuzikatae fedha hizi zinazopatikana kwa rushwa kwani ni sawa na kukumbatia dhambi,” alisema Sitta bila kuwataja wanaofanya hivyo.
Sitta ambaye ni Mbunge wa Urambo Mashariki alisema hakuna nchi iliyoendelea duniani kwa kukumbatia rushwa.
“Katika siasa hakuna mwanasiasa ambaye alianza siasa akiwa maskini na akatajirika kwenye siasa, ukiona hivyo huyo ujue ametuibia,” alisema Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa.
Alipoulizwa baadaye alikuwa anamlenga nani, alicheka, kasha akasema: “Ahaa, ni watu wa aina hii wako wengi, ni mtandao mkubwa.”
Kwa upande wake, Askofu Malasusa aliwaomba waumini kuwa wasilikizaji na washauri kuliko kutenda katika mtafaruku wa kidini unaondelea, ili kulinda amani iliyopo.
Katika harambee hiyo, Sh132 milioni zilipatikana ikiwa ni ahadi na fedha taslimu na kwamba kiasi kilichokuwa kinahitajika ni Sh200 milioni.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa, Mbunge wa Kahama, James Lembeli na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Margareth Sitta.

No comments:

Post a Comment