Wanaoipigia Kura CCM ni Kina Nani na Kwanini?
Hawa
watu wapo na bila ya shaka wana sababu. Wapo ambao wanaipigia kura CCM
na bila ya shaka wana sababu yao kama zao. Ni Watanzania – bila ya shaka
– na ni mamilioni – kwa uhakika – na hawa wanajitokeza siku ya kupiga
kura na kuchagua wagombea wa CCM na wanaichagua CCM. Swali ambalo labda
linahitaji utafiti wa kutosha ni kuwa hawa wapiga kura wanaoichagua CCM
au wanachagua mgombea wa CCM ni kina nani na wanafanya hivyo kwanini?
Unaweza kudhani CDM imeshawishi kila mtu Tanzania
Ukifuatia
na kusikiliza siasa za Tanzania unaweza kabisa kuamini kuwa CCM
inakaribia kufa na kama ingekuwa mgonjwa hospitali basi unaweza kudhania
yuko kwenye koma. Ni kama mgonjwa ambaye anajaribu kufufuliwa na
mashine huku roho ikiwa imeshikilia uzi tu! Jinsi ambavyo chama kikuu
cha upinzani nchini kinaonekana kuenea kila mahali, kikuvutia watu wa
kila hali, na kikijionesha ndicho pekee cha kweli ni rahisi kuamini
kabisa kuwa waliobakia CCM ni wabunge, madiwani, mabalozi na viongozi wa
waandamizi wa CCM. Lakini ukiangalia namba ni wazi lipo kundi kubwa –
na si dogo – ambalo bado linaamini, linakubali na liko tayari wakati
wowote ule kuchagua wagombea wa CCM na kuichagua CCM.
Fikiria:
Katika uchaguzi uliopita mgombea wa Urais wa CCM alipata kura
zisizopungua milioni 5 huku karibu asilimia 80 vya viti vya Ubunge
vikienda CCM! Sasa ni rahisi kusema kuwa kwenye Urais CCM walichakachua
kura lakini vipi kwenye Ubunge? Na hili tumeliona hata kwenye chaguzi
ndogo mbalimbali bado hata vijijini wapo wengi ambao ni mashabiki wa CCM
na ambao hawajashawishika na ujumbe wa CDM. Fikiria kule Arumeru
Mashariki ambapo Joshua Nassari na Sioi Sumari walikuwa wanapambana
Nassari alipata kura 32,972 wakati Sioi alipata 26,757; wote walipata
kwenye makumi elfu! Hawa watu ni kina nani na kwanini? Mfano mwingine wa
karibuni zaidi ni kuwa kwenye uchaguzi wa kata 22 uliofanyika mwezi
Juni CCM iliambulia viti 16 –japo ilipoteza kadhaa lakini kwamba bado
kuna watu walichagua madiwani wa CCM inabidi ipatiwe majibu.
Wanachagua Watu siyo Chama?
Inawezekana
mtu akasema hawa hawachagui chama wanachagua watu; jibu hili linavutia
lakini ni nani ambaye hajui kuwa watu wanawakilisha chama? Hakuna mtu
anayegombea kujiwakilisha yeye mwenyewe na kwa mfumo wetu ambao ni
lazima mgombea awe na chama ni wazi kuwa kuchagua mtu ni kuchagua chama
vile vile. Hivyo, ni vigumu sana kutenganisha kati ya kuchagua mtu na
kuchagua chama hasa kwa vile mtu aliyesimamishwa na chama anafanyiwa
kampeni na chama! Ni wazi kabisa kuwa japo wanaweza kuangalia mtu
anayegombea lakini mwisho wa siku wapiga kura wanajali ni chama gani
kimemsimamisha mtu huyo kwani baadhi ya watu ambao walitoka upinzani
walipoenda CCM na kusimama walishinda! – wapo wengine nao walikataliwa
ndani ya chama huko huko.
Hawaipendi na Kuikubali CHADEMA
Inawezekana
hili likawa jibu sahihi zaidi na kuukuu na kali; lakini laweza kuwa
ndilo la kweli zaidi. Kwamba, wapo mamilioni ya Watanzania ambao bado
hawajaamini, kuukubali au hata kushawishiwa na ujumbe wa CDM – kama
ujumbe huo upo. Siyo kwamba hawajausikia ujumbe wa CDM au hawaujui ni
kuwa hawajaukubali na haujawashawishi. Maelfu ya watu hawa wameona
maandamano, wameona majigambo na hotuba motomoto – Bungeni na nje ya
Bunge lakini mwisho wa siku wanasema hawajakubali. Kama hili ni kweli
swali hili basi ni muhimu zaidi kwa CDM kulitafutia jibu – kwanini wapo
watu ambao hawajakubali ujumbe wa CDM? Ni kwanini hawaikubali? NI kweli
wameaminisjwa ilwa CDM ni chama cha kidini, cha kikabila, cha kighaidi,
kinapenda fujo, au kuna kitu zaidi ya haya maneno ya propaganda; yaani
hawakubaliani na sera za CDM na mwelekeo wake?
Wananufaika na Utawala Uliopo?
Hili
nalo linaweza kuwa sehemu ya lile jibu sahihi. Kwamba maelfu ya watu
wanaopigia kura CCM na wagombea wake wanafanya hivyo kwa sababu chini ya
mfumo wa utawala wa sasa kundi hilo linanufaika. Inawezekana kuwa ni
manufaa ya kiuchumi – wafanyabiashara, wafanyakazi n.k au manufaa ya
kihisia (amani, umoja, na utulivu). Inawezekana pia ni watu ambao
wanaamini wataweza kufanikiwa zaidi chini ya CCM kuliko chini ya chama
kingine chochote kwa hiyo wao hawapigii kura matatizo yao ya sasa bali
matumaini ya maisha bora ya baadaye! Je inawezekana ndio maana asilimia
80 ya wapiga kura walimchagua Kikwete aliyekuja na “Maisha Bora kwa Kila
Mtanzania Yanawezekana”? Kwamba hawa hawakujali maisha yao duni, shida
zao na matatizo lukuki ambayo yapo; hawakujali ufisadi na madhara yake
na hawakujali mfumo wa kupendeleana sehemu mbalimbali; walichojali ni
kuwa labda huko mbeleni na wao watanufaika na hivyo wanapigia kura
maisha yao ya baadaye kuliko ya sasa (they are voting for their future
not their present)?
Kama
hili ni kweli, inawezekana kuwa CDM haijawapa matumaini kundi hili juu
ya maisha ya baadaye na wana hofu kuwa endapo CDM au chama kingine cha
upinzani kikiingia madarakani maisha ya kundi hili yanaweza yasiwe
mazuri sana au yatakuwa na mashaka? Inawezekana watu hawa wameamaini
kuwa amani, na utulivu vinawezekana tu chini ya
CCM na si chini ya chama kingine? Kama hili ni kweli CDM bado ina
maswali ya kujiuliza; je ifanye nini kushawishi kundi hili kuwa amani,
utulivu, na umoja utaendelea kuwepo nchini?
Hawa si Wasomi ni watu wa kijijini wanahitaji elimu zaidi
Mojawapo
ya majibu ambayo yanaweza kutolewa na baadhi ya watu kuwa hawa
wanaoichagua CCM hivi wengi ni watu wakijijini na labda si wasomi. Kwa
makosa watu wanaojenga hili wanataka tuamini kuwa wasomi ndio wanataka
mabadiliko zaidi! Hata hivyo ukiangalia utaona kuwa wasomi ndio
wananufaika zaidi na mfumo wa sasa chini ya CCM na wasomi wengi
wamekimbilia huko! Na ukiangalia mgawanyiko wa upigaji kura hasa kwa
baadhi ya maeneo utaona kuwa mabadiliko yamekubaliwa zaidi vijijini
kuliko mijini. Kama hoja ya usomi na kujua ingekuwa ina nguvu jiji la
Dar-es-Salaam lingekuwa na halmashauri zinazoogozwa na upinzani; hakuna!
Lakini ndio mahali penye vyuo vingi, shule nyingi, wasomi wengi na kwa
uhakika kabisa lenye fedha nyingi zaidi nchini na watu wake wanavyanzo
vingi zaidi vya habari lakini ndio wamekuwa wagumu zaidi kukubali
upinzani! Hata kwenye miji utaona ni miji michache bado ambayo imekubali
upinzani Arusha Mjini, Mwanza Mjini, Moshi Mjini, Mbeya Mjini, Iringa
Mjini, na Musoma Mjini. Sasa kwenye hii miji mingine kuna nini? Songea,
Morogoro, Dodoma, Tanga, Tabora, Shinyanga, n.k kunaninini? Lakini
ukiangalia vijijini upinzani unazama zaidi na zaidi; CDM inawabunge
wengi wa nje ya miji mikubwa kuliko wa mijini! Kwanini hasa?
Tungetarajia kuwa vijijini CDM isingeambulia hata mbunge au diwani mmoja
lakini tunaona imepata wabunge na madiwani hadi sehemu ambazo
haikufanya kampeni sana; fikiria Ukerewe na Maswa Mashariki! Kwanini
siyo Temeke, au Ilala; au Morogoro Mjini?
Maswali
haya yanahitaji majibu; je ni kwa sababu CCM inafanya vizuri sana
kuliko CDM au kwa sababu kuna mbinu nyingi chafu zinazofanya CDM
kujipenyeza mijini kuwa ni ngumu zaidi kuliko vijijini. Katika kutafuta
majibu ya maswali haya ndio ufunguo wa nani atashinda 2015 umejificha.
CDM haipaswi kutegemea kura za chuki dhidi ya CCM kuwa ni kura za
mapenzi kwa CDM; hatari yake ni kuwa CCM ikifanya vizuri watu ambao
walikuwa hawajafanya uamuzi bado ni rahisi kusema tujaribu nao tena. Kwa
mfano Dar patakuwa pagumu sana kwenda 2015 baada ya kukamilika kwa
mradi wa DART, kukamilika kwa Daraja la Kigamboni na kuboresheka kwa
usafiri wa treni! Na tunavyojua jinsi CCM inavyojua kutumia miradi ya
miundombinu kama kete kuelekea 2015 kutakuwa na shambulio la ukarimu
hadi kwenye majimbo ya wapinzani; na wapo watakaoshawishika.
Wapo Wenye Mapenzi ya Dhati na CCM?
Jibu
jingine ambalo linaweza pia kuwa ni la kweli zaidi ni kuwa wapo maelfu
kama siyo mamilioni ya Watanzania ambao kwa sababu zao wenyewe wana
mapenzi ya dhati kabisa kwa Chama cha Mapinduzi na hakuna lolote au
chochote ambacho CCM inaweza kufanya kikaondoa mapenzi hayo. Hawa
inawezekana kabisa wanatambua matatizo ya CCM na utawala wake lakini
kama vile mapenzi ya mtoto kwa mzazi ndivyo nao walivyo; wanaipenda CCM
kwa sababu hawawezi kupenda kwingine! Wao wanaamini wakati huu ambapo
CCM inapitia wakati mgumu zaidi ndio wakati wa kuonesha mapenzi zaidi
kwa CCM kwani wanaamini mambo yakitulia basi na wao watanufaika na nchi
itanufaika. Kama kundi hili ni kubwa ndani ya lile linalopigia kura CCM
sijui; lakini kama kweli lipo na lina nguvu basi hili ni kundi
litakalosumbua sana upinzani na hasa CDM; hawa hawajali CDM inasema
nini, inapigania nini, inawakilisha nini, kwa nini, wapi, na kwa vipi!
Wao wanachojali ni kuwa CCM iendelee kutawala na hata ikiwezekana hadi
qiyama.
Lakini
bado swali hili linahitaji majibu na yeyote mwenye majibu atushirikishe;
nitayapost majibu mbalimbali kwenye blog hapa: Andika jibu lake – si
zaidi ya kurasa moja (1) ukijibu swali hili: Hawa wanaopigia kura CCM ni
kina nani hasachanzo http://www.mwanakijiji.com
No comments:
Post a Comment