Kwaheri Tendwa, tutakukumbuka kwa ulivyotenda; Uishi na Afya Uone Nchi Ikirudishwa kwa Wananchi!
Tendwa atakumbukwa kwa mengi lakini kwa kiasi kikubwa kwa kuonekana kuwa ni kibaraka asiyechoka wa chama tawala na wa mfumo wa kisiasa ulioshindwa. Atakumbukwa kwa kutumia nafasi yake kufanya shughuli za siasa nchini kuwa ngumu, za upande mmoja na zisizo na usawa wowote. Tutamkumbuka zaidi kwa kushindwa kusimamia sheria ya Vyama vya Siasa na hasa sheria ya fedha za kampeni za kisiasa. Chini ya uongozi wake tumeshuhudia dola ikijisimika zaidi na zaidi katika siasa huku wanasiasa wachama tawala wakitumia nafasi wazipatazo kukandamiza upinzani nchini huku Tendwa – mwamuzi wa siasa nchini – akitoa maneno yenye kujiuma uma na kujikanyaga ambayo yaliashiria kujikomba mbele ya watawala.
Wakati wa Tanzania tunafurahia kuondoka kwa bwana huyu tunajua kabisa zamu yake ya kupewa shukrani inakuja na kwa hakika atapewa shukrani fulani kwani hataachwa astaafu na yeye kuonja machungu ya wastaafu wengine nchini. Watawala ni lazima washukuru kwani yeye pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kwa muda mrefu Jaji Lewis Makame walishiriki -kwa kujua au kutokujua – kudumaza mwamko wa demokrasia hasa katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 na chaguzi ndogo zilizofuatia. Tayari Tume ya Uchaguzi ilipata Mwenyekiti Mpya Jaji Damian Lubuva na tayari utendaji wa tume yake haujawa na tofauti kubwa na ule wa Makame.
Ujio wa Msajili Mpya Jaji Francis Mutungi kunapaswa kuangaliwa kwa hali ya mashaka na shuku. Kwa vile tunatambua kuwa Msajili huyu anaingia chini ya mfumo na sheria ile ile ya vyama vya siasa ni wazi kuwa bado anafungwa na mfumo mbovu ule ule ambao haujatengenezwa kuhakikishwa uhuru wa kisiasa, usawa na uwajibikaji. Yeye naye akiongozea na mapenzi binafsi kwa chama chochote cha siasa anaweza kuwa kikwazo kwa ukuaji wa demokrasia nchini.
Kazi kubwa ambayo inahitajika kufanywa na wanaharakati sasa hivi ni kuanzisha shinikizo la mabadiliko katika sheria zinazohusiana na siasa nchini ili kuhakikisha kuwa kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani na kabla ya kura ya maoni ya katiba mpya na uchaguzi mkuu wa 2015 mabadiliko ya msingi yanafanyika katika sheria hizi ili kuhakikisha usawa, uwazi, uwajibikaji na maadili bora katika siasa za nchi yetu. Tusije kuishia kuwalalamikia wanaoshika usukani wakati kilichoharibika ni gari lenyewe!
Ninamtakia Bw. Tendwa maisha mema ya kustaafu na kumwombea afya ili aishi na kuona mabadiliko ya kweli katika siasa za Tanzania, aone weledi katika cheo hicho na zaidi aone Watanzania wakitumia njia za amani wakiwaondoa watawala walioshindwa na kuingia utawala mpya wa kisiasa ambao utabadili siyo tu sura za watawala bali mfumo mzima wa utawala na hivyo kulirejeshia taifa letu mikononi mwa wananchi na kulipokonya kutoka katika kucha kali za watawala walioshindwa.
Kwa Jaji Franchi naweza kusema moja tu; hatutampima kwa maneno yake au kwa ahadi zake; hatutampika mwa aliyoyafanya huko nyuma au aliyoshindwa kufanya kwani sasa hivi atapimwa kwa ofisi yake hii mpya kwa yale atakayoyatenda. Tunasubiri kwa hamu kuona kama hatimaye ofisi hiyo imepata mtu anayeimudu kweli au utakuwa ni mwendelezo wa watu wale wale ambao wanajifikiria miungu watu ambao wanatamani watu wawafukuzie uvumba na manukato wakitoa sadaka za sifa kwenye madhabahu ya wanasiasa.
Muda utaamua.
No comments:
Post a Comment