Upinzani ‘wawasha moto’ Zanzibar,wataka Chikawe ajiuzulu kwa taarifa za uongo
Waziri wa
Sheria na Katiba Mathias Chikawe ametakiwa ajiuzulu kwa kutoa taarifa za
uongo kwamba Zanzibar ilishirikishwa kabla ya Muswada wa Mabadiliko ya
Katiba kuwasilishwa bungeni na kupitishwa na Bunge Septemba mwaka huu.
Msimamo huo
ulitolewa na Waziri wa Sheria na Katiba Zanzibar, Aboubakary Khamis
Bakari wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliovishirikishwa vyama vya
Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi uliofanyika Uwanja wa Kibandamaiti mjini
Unguja jana.
Aboubakari
alisema kwamba Zanzibar ilipokea taarifa ya awali ya mabadiliko kuhusu
vifungu vinne vya Muswada wa Mabadiliko ya Katiba na kutakiwa Zanzibar
itoe maoni na mapendekezo yake, jambo ambalo alisema lilifanyika kupitia
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Hata hivyo,
alisema vifungu vya mabadiliko ghafla viliongezwa kutoka vinne hadi 12
bila ya Zanzibar kupewa nafasi ya kujadili vifungu vinane ambavyo vina
umuhimu mkubwa katika kupata katiba bora.
“Waziri nimesoma naye Chuo Kikuu mwaka 1972, Chikawe kwa hili amesema uongo vinginevyo ajiuzulu, hafai,” alisema Aboubakari.
Alisema
kabla ya kufanyika Waziri akifuatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulikia Bunge, William Lukuvi walifika Zanzibar na kutaka
wajadili vifungu hivyo kwa siku moja jambo ambalo alipinga kulitekeleza.
“Baada ya
kuanza kupiga kelele, wenzetu walikuja Zanzibar wakitaka tujadili
mabadiliko ya mswada,nikawaambia siwezi kujadili masilahi ya nchi
kijuujuu, huko ni kuiuza nchi, siko tayari kufanya hilo,” alisema.
Aboubakari
alisema marekebisho yaliyofanyika katika muswada huo na kutoa nafasi
kujadili na kupitisha mabadiliko ya Katiba kwa kutumia wingi wa kura ni
sawa na wazimu.
Alisema
mabadiliko yoyote ya Katiba yanapaswa kutumia theluthi mbili toka pande
mbili za Muungano, utaratibu ambao ndiyo umekuwa ukitumika na nchi
mbalimbali zenye mfumo kama wa Tanzania. Mwananchi ilipomtafuta Waziri
wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe kujibu tuhuma hizo alisema
Aboubakari ameudanganya umma mchana kweupe kwa vile yeye na Waziri
Lukuvi walifika Zanzibar kupeleka rasimu ya muswada na si kujadili na
kupokea mapendekezo papo kwa hapo.
Chikawe
alisema kwamba walipokabidhi muswada pia walimtaarifu siku ya
kuwasilishwa muswada huo katika kikao cha Bunge na kuwataka kutoa maoni
na mapendekezo kwa wakati mwafaka kabla ya kujadiliwa na kamati ya
Katiba ya Sheria ya Bunge.
Alisema
kwamba nyongeza ya marekebisho ya vifungu vinane yalitokana na
mapendekezo ya wabunge katika kamati na michango ya wabunge ndani ya
Bunge katika utaratibu unaoruhusiwa kisheria.
“Baada ya
kamati ya Bunge kukaa, Mbunge Halima Mdee wa Chadema ndiye
aliyependekeza kutumika kwa utaratibu wa wingi wa kura katika kupitisha
mabadiliko hayo ya Katiba kama hatua ya theluthi mbili itashindwa
kufikia mwafaka,” alisema Chikawe.Pia
alisema mbunge kupitia Baraza la Wawakilishi, Jaku Hashim Jaku yeye
alitetea kwa nguvu ya hoja kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba imalize
kazi yake baada ya kuwasilisha ripoti yake kwa Rais na kwamba haikuwa ni
uamuzi na matakwa ya Serikali kama inavyodaiwa na vyama vya upinzani
kuhusu nyongeza hiyo.
“Nyongeza ya
vifungu ilitokana na wabunge katika kamati na ndani ya Bunge lenyewe,
Serikali haiwezi kupuuzia ushauri wa wawakilishi wa wananchi na wabunge
ambao wanaisimamia Serikali,” alisema Waziri Chikawe.
Aidha,
Aboubakari alimshutumu Naibu Spika wa Bunge,Job Ndugai kwa kulidanganya
Bunge kwa kitendo chake cha kutoa barua ikithibitisha Zanzibar
imeshiriki wakati kuna vifungu vya ziada vimefanyiwa marekebisho bila ya
kupata baraka ya Zanzibar.
Alisema kwa
msingi huo amevunja na kukiuka kanuni za Bunge na wabunge wana haki ya
kumshtaki kwa kutumia kanuni zao kwa kupotosha Bunge na umma.
Hata hivyo,
taarifa hizo za Aboubakari kutokana na maelezo aliyotoa awali Katibu
Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kwenye mkutano wa hadhara, alisema
Zanzibar ilishirikishwa katika kuvifanyia vifungu sita na SMZ ilitoa
mapendekezo katika vifungu vitatu na baadae vikaongezwa vinane kinyemela
bila ya Zanzibar kushirikishwa.
Kwa upande
wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kwa muda mrefu
viongozi wa Zanzibar walikuwa wakijitolea kupigania mabadiliko ya taifa
lao na kukutwa na vizingiti ikiwemo kuwekwa vizuizini na kupewa hongo ya
madaraka.
Mbatia
alisema miongoni mwa viongozi waliojitoa muhanga kutaka mabadiliko ya
mfumo wa Muungano ni pamoja na Rais wa Awamu ya Pili Zanzibar, Aboud
Jumbe Mwinyi ambaye aliondolewa kibabe madarakani chini ya uongozi wa
Mwalimu Julius Nyerere.
Naye
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alimtaka Rais Jakaya Kikwete
kumfuta kazi Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema na Waziri wa
Katiba na Sheria, Mathias Chikawe kwa madai kuwa hawana nia njema
wakikusudia kuharibu nia njema ya Rais ya kupata Katiba mpya.
Mwenyekiti
wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema Katiba iliyopo sasa nchini
haifai kwa kuwa imejaa upungufu unaokwenda kinyume na misingi ya haki za
raia
No comments:
Post a Comment