SIKU chache baada ya Waziri wa zamani na Mbunge wa Urambo Magharibi,
Profesa Juma Kapuya (CCM) kutuhumiwa kumbaka na kutishia kumuua binti
mdogo wa miaka 16, kiongozi huyo ameibuka na kutoa utetezi wa
kujikanganya.
Akizungumza kupitia kwa wakili wake, Yasin Memba, mbunge huyo alitishia
kuliburuza gazeti hili mahakamani endapo halitamwomba msamaha ndani ya
siku saba.
Pamoja na kukataa kwake kumfahamu binti huyo, Kapuya amekiri kumiliki
simu namba 0784993930 ambayo imekuwa ikitumiwa kuwasiliana naye ikiwemo
kumtumia ujumbe mfupi wa maneno (sms) wa vitisho.
Hata hivyo, katika namna ya kushangaza, Kapuya alidai kwamba simu hiyo
aliishaigawa miezi sita iliyopita, na hivyo hausiki kwa namna moja ama
nyingine na tuhuma alizopewa.
Lakini wakati Kapuya akikwepa mtego huo, Novemba 9, mwaka huu, gazeti
hili liliwasiliana naye kupitia namba hiyo hiyo anayodai kwamba
alishaigawa miezi sita iliyopita.
Tarehe hiyo, gazeti hili liliwasiliana na mbunge huyo ili kuthibitisha
tuhuma zilizokuwa zikimkabili wilayani Kaliua za kumpiga makofi kiongozi
mmoja wa CCM.
Kapuya kupitia namba hiyo, alitoa utetezi wake ambapo gazeti hili lina sauti yake.
Utetezi wake pia unaongeza utata kwani hakufafanua ilikuwaje akagawa
namba ya simu iliyosajiliwa kwa jina lake kwa mtu mwingine, huku
ikiendelea kutuma fedha na vitisho kwa binti huyo.Katika utetezi wake
jana, Kapuya alikana kutomjua binti huyo wala dada yake, na kwamba yeye
si mwathirika wa ugonjwa wa ukimwi.
Alilishutumu gazeti hili kuwa lilijifanya hakimu kwa kuchapisha tuhuma
zake bila kumpa nafasi ya kujitetea kama ilivyo kawaida kwenye tasnia ya
habari.
Hata hiyo, ukweli ni kwamba nafasi hiyo aliipata, lakini hakuitumia
kwani alipopigiwa, simu yake ilipokelewa na mtu aliyejitambulisha kuwa
ni dereva wake na kutaka aelezwe sababu za kutafutwa bosi wake.
Hata alipoelezwa kuwa anayehitajika ni bosi wake, alisita kisha alitoa
namba nyingine ya simu akitaka atafutwe kupitia namba hiyo.
Lakini muda wote namba hiyo haikupokelewa na hata alipopigwa tena namba ya awali, nayo iliita bila kupokelewa.
Wakili Memba alidai kuwa mteja wake, alimweleza kuwa habari ile
imemletea madhara na usumbufu mkubwa katika familia yake, jamii na
kumvunjia heshima yake.
"Kwa sababu hiyo, amenielekeza niwapatie siku saba gazeti la Tanzania
Daima, mitandao ya kijamii ukiwemo wa Jamii Forum, Justina John na
Vituko Mtaani ambao walichapisha habari hiyo, waombe radhi kwa uzito ule
ule la sivyo atavishitaki mahakamani.
"Kama hawataomba radhi, basi atafungua kesi mbili, moja ni kwa ajili ya
gazeti la Tanzania Daima na hiyo mitandao ya kijamii, na kesi ya pili ni
ya kuhusu huyo mtoto anayedaiwa kubakwa na kuambukizwa ukimwi,"
alisema.
Aliongeza kuwa wanataka mtoto huyo aje mahakamani athibitishe
aliambukizwaje ukimwi na alete ushahidi unaoonyesha Kapuya ana ukimwi.
Memba aliuomba umma kuelewa kuwa habari hiyo iliyochapishwa na Tanzania Daima haiusiani na chama chake wala serikali.
Kwa siku mbili mfululizo gazeti hili lilifichua tuhuma za Kapuya kudaiwa
kumbaka mtoto huyo, na hata baada ya kubaini siri hiyo imevuja,
alimpigia simu mtoto huyo, na baadaye kutuma meseji kadhaa za vitisho.
Tanzania Daima ilishuhudia baadhi ya meseji za simu zilizotumwa na Prof.
Kapuya kwenda kwa mtoto huyo.Juzi alfajiri saa 11:21 kupitia simu yake
alituma ujumbe kwa mtoto huyo: "Chagueni kunisubiri tuje tuongee au
mnataka kufa?"
Baadaye saa 1:07 asubuhi, alituma ujumbe mwingine kutoka simu hiyo hiyo
kwenda kwa mtoto huyo, ukisema: "Mkiuawa, itakuwa nzuri, itawapunguzia
gharama za kuishi. Usitake kugombana na serikali, mtoto mdogo kama wewe.
Sisi ndo wenye nchi yetu."
Baadhi ya mashirika yanayotetea makundi kadhaa yakiwamo Kituo cha Sheria
na Haki za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP)
yalijitokeza kuwasaidia watoto hao, ambao ni yatima.
Mtoto huyo na dada yake, wakizungumza na gazeti hili kwa hofu mafichoni,
walisema kwa sasa hawana imani tena kama kuna serikali nchini Tanzania
kwa kuwa wamedhalilishwa, wametembezwa hadi bungeni na wabunge bila
hatua kuchukuliwa, licha ya kutoa taarifa katika Kituo Cha polisi
Oysterbay tangu mwaka jana.
Hata hivyo, kabla ya tukio la watoto hao kuripotiwa ofisi za gazeti
hili, juzi usiku kulikuwa na watu waliokuja wakiwatafuta watoto hao,
huku wakiwatisha kwa simu na kuwatolea maneno ya kejeli, wakidai
watawamwagia tindikali.
Juzi gazeti hili lilichapisha habari kuhusu mwanafunzi huyo aliyesema
kuwa waziri huyo alimbaka kwenye hoteli moja ya kitalii iliyoko jijini
Dar es Salaam mwaka 2011, na kurudia tena kitendo hicho katika Jengo la
Biashara Complex lililoko Mwananyamala Juni 3, 2012 alipoitwa kwenda
kuchukua ada kwa mara ya pili.
CHANZO:http://www.jamiiforums.com/
No comments:
Post a Comment