MAPYA YAIBUKA TENA Baada ya Kikombe cha Babu, dhahabu yaibuka Samunge.
Arusha. Maelfu ya watu wamemiminika tena katika eneo la Samunge, Wilaya ya Ngorongoro Mkoa wa Arusha, safari hii siyo kunywa Kikombe cha Babu Mchungaji Ambilikile Mwasapile, bali kupata dhahabu inayodaiwa kugundulika katika eneo hilo.
Habari kutoka katika eneo hilo zinasema kuwa watu wanazidi kumiminika
katika kujipatia madini hayo yaliyobainika katika mashamba ya watu na
maeneo ya kingo za Mto katika Kijiji cha Mgongo kilichopo jirani na Kwa
Babu.
Diwani wa Samunge, Jackson Sandea alisema maelfu ya watu kutoka
maeneo mbalimbali nchini wamefurika katika kijiji ambacho kuna mto na
madini ya dhahabu yanapatikana hapo.
“Hadi sasa kuna watu zaidi ya 4,000 na bado wanaongezeka, hii inaweza
kuwa ni zaidi ya kipindi kile cha Babu wa Kikombe. Dhahabu hii
inapatikana mtoni tu, watu wanakusanya michanga na kupata dhahabu,
hakuna mtu ambaye anachimba,” alisema Sandea.
Alisema tofauti na maeneo mengine, dhahabu ya Samunge inaonekana ni
ya Watanzania wote kwani ipo eneo la mto ambao unamilikiwa na Serikali
na ndiyo sababu watu wanaingia kwa wingi.
“Kuna wengine wanapata hata mashambani lakini mtoni ndipo inapatikana kwa wingi zaidi,” alisema.
Ulinzi waimarishwa
Diwani huyo alisema ulinzi umeanza kuimarishwa katika eneo hilo
akisema hali ikiachwa kama ilivyo, kunaweza kutokea vurugu kubwa na hata
mauaji.
“Sisi kama viongozi, tumeweka utaratibu mzuri wa kuchimba madini
kiusalama na hata wale ambao wameanza kuuza mashamba yao, tunawawekea
utaratibu mzuri,” alisema.
Maofisa madini kutua Samunge
Kamishna wa Madini Kanda ya Kaskazini, Alex Magayane alisema jana
kwamba baada ya kupokea taarifa za kugundulika kwa dhahabu katika eneo
la Samunge, maofisa wake wanajiandaa kwenda kijijini hapo.
Alisema taarifa za kitaalamu kuhusu akiba ya madini hayo iliyopo
Samunge itatolewa baada ya maofisa hao kufika katika eneo hilo na
kufanya utafiti.
No comments:
Post a Comment