Afisa
Mnadhimu namba wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa
Polisi (ACP) Japhet Lusingu akitoa ufafanuzi wa mada mbalimbali
zilizojadiliwa kati ya Jeshi hilo na wadau wa Polisi Jamii Mkoa wa
Arusha katika kikao kilichofanyika ukumbi wa Bwalo la Afisa wa Polisi
(Police Officers Mess) mwishoni mwa wiki. Picha na Rashid Nchimbi wa
Jeshi la Polisi Arusha.
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha.
Wadau
wa Polisi Jamii Mkoa wa Arusha kutoka kada mbalimbali wakiwemo
wanasheria, wafanyabiashara na wafanyakazi kutoka sekta binafsi na za
kiserikali wamedhamiria kufungua Akaunti benki kwa ajili ya kuliwezesha
Jeshi la Polisi katika kupambana na uhalifu.
Hayo
yalielezwa na wadau hao wakati wa kikao cha kujadili usalama wa mkoa
huu kilichofanyika kwenye Bwalo la Maofisa wa Polisi (Police Officers
Mess) mwishoni mwa wiki kati yao na Viongozi wa Jeshi la Polisi mkoani
hapa. Wadau hao walisema kwamba wawezeshaji wa Jeshi hilo ni wana Arusha
wenyewe hakuna mtu yeyoye atakayetoka mkoa mwingine kwa ajili ya
kuliwezesha Jeshi la Polisi mkoani hapa.
“Tunataka Arusha
iwe mfano na mikoa mingine iige, bila kuwawezesha Polisi hatuwezi
kukomesha uhalifu na tunatakiwa tuwawezeshe ili tupate nafasi ya
kuwalaumu, hivyo basi nashauri iundwe Kamati ndogo itakayowajumuisha
Polisi na Wananchi ambao watafanya harambee kwa watu mbalimbali”.
Alisema Kiomoni Kibamba ambaye ni Mwanasheria wa Halmashauri ya jiji la
Arusha.
Wadau hao walisema pamoja na Mfuko huo kutumika
kuliwezesha jeshi la Polisi katika kuongeza bajeti ya mafuta na vifaa
vingine lakini pia utakuwa unatumika kuwapa motisha wale wote
watakaokuwa wanaliwezesha Jeshi hilo kuwapa taarifa za uhalifu na
wahalifu ili kuonyesha kuwa wanathamini mchango wao.
Mbali
na mada mbalimbali zilizokuwa zinajadiliwa siku hiyo pia wadau hao
walilishauri Jeshi la Polisi Mkoani hapa kuwa makini na waendesha
pikipiki yaani Boda Boda na ikibidi kila pikipiki inayotumika
kusafirisha abiria iwe na makazi ya maegesho yanayojulikana ili tukio la
uhalifu linapotokea askari wawe wanapata pa kuanzia katika suala zima
la upelelezi.
Walisema kwa sasa pikipiki hizo zinafanya kazi
mpaka usiku hivyo kama kuna uwezekano wangewekewa ukomo hasa muda wa
usiku badala ya kufanya biashara hiyo mpaka asubuhi kwani baadhi yao
wanatumia mwanya huo na kujiingiza katika vitendo vya kihalifu.
Awali
akifungua kikao hicho Katibu wa kikao hicho Bw. Adolph Olomi ambaye
pia ni Mwenyekiti wa TCCIA mkoa wa Arusha, alisema kwamba pamoja na
mambo mengine lakini pia lengo la mkutano huo ni kufahamiana ili
kupunguza kama si kuondoa kabisa pengo kati Jeshi hilo na wananchi hali
ambayo itasaidia kuwa na ukaribu utakaosaidia kushughulikia matatizo ya
kihalifu kabla hayajatokea.
Kwa upande wake Afisa Mnadhimu
namba moja wa Jeshi hilo mkoani hapa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP)
Japhet Lusingu aliwataka wadau hao watoe taarifa za wahalifu na uhalifu
kupitia kwa viongozi wa Jeshi hilo ili kupunguza malalamiko juu ya
uvujaji wa taarifa hizo.
(ACP) Lusingu aliongeza kwa kusema
kwamba, hata watoa taarifa mara baada ya kutoa taarifa Polisi wanatakiwa
wakae kimya bila kumshirikisha mtu yeyote kwani hali hiyo inasababisha
majirani kumfahamu mtoaji wa taarifa hizo na baadae wahalifu kumfahamu
kisha lawama kuliangukia jeshi la Polisi hivyo akasisitiza kwamba usiri
unatakiwa kuanzia kwa mtoa taarifa mwenyewe.
Akitoa mada
katika kikao hicho Mkuu wa kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha
Mrakibu Mwandamizi (SSP) Mary Lugola alisema kwamba, umefika wakati
muafaka kwa Jeshi la Polisi na wananchi wote kufanya kazi kwa ukaribu
zaidi ili kuweza kuimarisha usalama. Alisema kikao hicho ni moja ya
mpango mkakati wa kuhakikisha mkoa wa Arusha unakuwa salama hasa
ikizingatiwa pia ni kitovu cha shughuli za kitalii.
Naye
Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha Mrakibu wa Polisi (SP) Francis Duma
alisema kwamba, Falsafa ya Polisi Jamii ilikuja baada ya kuona kuna
pengo kubwa kati ya Polisi na Jamii hivyo kuondoshwa kwa pengo hilo
kumesaidia pande hizo mbili kuwa karibu.
Alisema Polisi
pekee bila kushirikiana na wananchi haiwezi kukomesha uhalifu
ikizingatiwa kwamba, kutokana na sensa ya mwaka 2012 uwiano unaonyesha
kuwa, Polisi mmoja anatakiwa ahudumie kaya 1300 kwa masaa 24 bila
kupumzika, hivyo ukomeshaji wa matukio ya uhalifu utafanikiwa endapo
wanajamii nao watajitoa ipasavyo katika suala zima la kuimarisha
usalama.
No comments:
Post a Comment