Jaji Warioba amjibu Bulembo (CCM)
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba amesema
baadhi ya wanasiasa wameacha kujadili rasimu ya Katiba iliyotolewa na
Tume yake badala yake wamejikita katika kuijadili Tume yake na Wajumbe.
Kauli ya Jaji Warioba imekuja kufuatia tuhuma zilizotolewa na Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Bw. Abdallah Bulembo
mkoani Tanga zilizonukuliwa na ITV na baadhi ya magazeti leo.
Katika taarifa hizo, Bulembo anaelezwa kusema kuwa Tume ya Warioba
imekuwa ikiingilia uhuru wa wananchi kutoa maoni katika mikutano ya
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya badala ya kukusanya maoni ya wananchi hao
na kuongeza ikiwa Tume au Jaji Warioba anataka kufanya kazi hiyo, basi
ajiuzulu kwanza katika Tume.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa akizungumza jijini Dar es Salaam leo,
Warioba, ambaye ameshawahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri
Mkuu, amesema kauli hizo ni upotoshaji na kuwa Tume yake ina jukumu la
msingi la kutoa elimu kwa umma.
“Moja ya kazi za kisheria za Tume ni kutoa elimu kwa umma, na ni kazi ya
wakati wote,” anaelezwa kusema Jaji Warioba wakati akijibu swali la
mwandishi mmoja kutoka Star TV aliyeongozana na baadhi ya waandishi
wengine kutoka ITV, Channel Ten na Clouds FM.
Kwa mujibu wa Warioba, katika mikutano ya Mabaraza ya Katiba ya Wilaya,
wananchi ambao walikuwa ni wajumbe wa Mabaraza hayo walikuwa na fursa ya
kuuliza maswali na Wajumbe wa Tume walitoa elimu kuhusu hoja na maswali
yaliyoulizwa kwa mujibu wa sheria.
“Sasa anaona (Bw. Bulembo) kuwa kutoa elimu ni dhambi,” alisema
Mwenyekiti huyo na kuongeza kuwa hii sio mara ya kwanza kwa Bulembo
kutoa kauli kama hizo.
“Nilimsikia Mbeya, Moshi na sasa Tanga akitoa matamshi hayo… kwa kawaida
huwa sizungumzii mambo haya, huwa tunayaacha yapite,” alisema na
kufafanua kuwa kauli kama hizo zimekuwa zikiwafanya wajumbe wa Tume
kufanya kazi katika mazingira magumu.
“Nilisema katika mkutano wangu na waandishi wa habari mwishoni mwa mwezi
uliopita kuwa Tume yake imekuwa ikifanya kazi katika mazingira magumu
kutokana na kauli za wanasiasa, zikiwemo zake (Bulembo),” alisema na
kuongeza kuwa, pamoja na kauli hizo, Tume yake inafarijika na kauli za
kutia moyo wanazozipata kutoka kwa wananchi wa kawaida.
“Matamshi mengine yalilenga Tume na wakati mwingine yalinilenga mimi
binafsi au wajumbe wa Tume badala ya kuzungumzia rasimu,” anaelezwa
kusema.
Jaji Warioba alisema Tume yake siku zote imekubali kukosolewa kwa
kuamini kuwa kukosolewa ni jambo la kawaida lakini akaongeza kuwa ni
vema wananchi na wanasiasa wakajadili rasimu ya katiba iliyotolewa
badala ya watu au Tume.
“Nadhani wangezungumzia rasimu wangetusaidia sana, badala ya kuzungumzia Tume na watu,” amesema Jaji Warioba.
Kuhusu kujiuzulu, Jaji Warioba anaelezwa kusema kuwa haamini kuwa kauli
zinazotolewa na Bulembo ni kauli za CCM kwa kuwa CCM haijawahi kuitaka
Tume ijiuzulu.
“Sina hakika kama anazungumza kwa niaba ya CCM kwani CCM haijasema tujiuzulu,” anadaiwa kusema.
CHANZOhttp://www.jamiiforums.com
No comments:
Post a Comment