UKAWA WASUSIA BUNGE MAALUM LA KATIBA
Mjumbe
wa Bunge Maalumu la Katiba, Prof Ibrahimu Lipumba akizungumza katika
kikao cha bunge jana ambapo alitangaza kujitoa kwa baadhi ya wajumbe
kuendea na mchakato wa kupitisha Rasimu ya Katiba, mjini Dodoma jana.
Picha na Edwin Mjwahuzi
Dodoma. Mambo
yamebadilika. Ukimya ulitawala jana katika Ukumbi wa Bunge mjini Dodoma,
baada ya wabunge zaidi ya 200 ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), kususia vikao vya Bunge hilo.
Ilikuwa ni saa 10:31 jioni baada ya Mjumbe wa Bunge hilo ambaye pia
ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alipohitimisha uchangiaji
wake akisema: “Ukawa hatuwezi kuendelea kushiriki dhuluma dhidi ya
wananchi kwa kupitisha Katiba ambayo ni kinyume cha matakwa yao.”
Baada ya kauli hiyo aliondoka akifuatiwa na Mwenyekiti wa Ukawa
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR
Mageuzi, James Mbatia na wajumbe wao kutoka nje ya Bunge.
Ukimya ulitawala
Baadaye aliliambia Bunge kuwa makatibu wamemweleza hawahitaji akidi
kwa kuwa kikao kilikuwa kinaendelea wakati Ukawa walipotoka nje ya
ukumbi.
Hotuba ya Lipumba
Profesa Lipumba alianza kwa kunukuu Gazeti la Mwananchi la Aprili 14,
mwaka huu katika sehemu inayosema; “Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge) ameanza kampeni kanisani kwa kuwataka
wananchi kupinga serikali tatu zilizopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, vinginevyo nchi itatawaliwa na jeshi kwa kuwa serikali ya
muungano itashindwa kuwalipa mishahara wanajeshi.”
Alisema yeye ni muumini wa dini ya Mwenyezi Mungu lakini anaafiki
mapendekezo yaliyoletwa bungeni hapo na Tume ya Mabadiliko ya Katiba
iliyoundwa na Rais.
“Hii ni kauli ya Waziri Lukuvi ndani ya Kanisa la Methodist wakati wa
sherehe ya kumsimika Mchungaji Joseph Bundala kuwa Askofu na Waziri
Lukuvi alikuwa anamwakilisha Waziri Mkuu.”
Alisema inasikitisha kwa sababu kauli hiyo inafanana na ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa wakati akihutubia Bunge Maalumu.
Alisema kauli za Lukuvi zinatisha baada ya kusema Wazanzibari ambao
wanataka kuwa na nchi yao hawawezi kujitegemea, bali wanataka wapate
nafasi ya kujitangazia kuwa ni nchi ya Kiislamu.
“Waziri anaweza kusema hivyo ndani ya kanisa? Kawahamasisha mpaka
yule kiongozi wa kanisa akasema ili kudumisha Muungano bora Katiba ya
Zanzibar ifutwe ili iwepo moja ya nchi moja ambayo inadumisha Muungano,”
alisema.
Alisema Lukuvi alikuwa akiwaaminisha kuwa mfumo wa serikali tatu
ukipita kutakuwa na mapinduzi na nchi haitatawalika na hivyo watu
watashindwa kwenda kusali makanisani.
“Kama ndugu zetu wa Zanzibar wangekuwa wanahitaji serikali moja
tungekuwa na utaratibu mzuri tu, lakini siyo wanachama wa CUF, siyo wa
CCM, Wazanzibari wote hawataki muungano wa serikali moja,” alisema.
Alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa mapendekezo ya serikali
tatu kutokana na ukweli huo. “Hoja zilizoletwa hapa ni hoja za serikali
moja, si hoja za serikali mbili lakini wenzetu moja hawataki, kwa hiyo
tunahitaji Muungano ambao tutakuwa na maridhiano ya pande zote mbili,”
“Wengi wamenukuu makala niliyoitoa katika kituo cha TCD (Kituo cha
Demokrasia Tanzania), ambayo iliunda Baraza la Katiba na mimi
nilichambua mapendekezo ya Tume nikasema kwa mapendekezo yaliyomo ndani
ya Rasimu ya Katiba hayatakidhi mapato ya shirikisho.”
Alisema wajumbe wanaomnukuu wanaishia hapo bila kwenda katika mapendekezo aliyoyatoa.
“Wamenisifu sana ni mchumi mahiri, basi waendeleze sifa hizo kwa
mapendekezo niliyoyatoa ya mapato ya kukidhi uendeshaji wa serikali ya
shirikisho.
“Nimeeleza katika hali halisi kuwa utaratibu mzuri ni mapato ya kila
serikali kuchangia katika shirikisho na mambo haya yaandikwe katika
Katiba. Katiba inaweza ikasema wazi asilimia 20 ya mapato yote
yanayokusanywa Zanzibar au Tanganyika yataenda kwenye shirikisho.”
Alitaka pia kuwekwa kwa misingi mizuri ya kukusanya kodi na kutumia
fedha za wananchi ndani ya katiba ya muungano ambayo ndiyo katiba mama.
“Lakini ndugu zangu mjadala wetu unavyokwenda utadhani kuwa Rasimu ya
Katiba iliyoletwa imeletwa na CUF au na Chadema au na NCCR-Mageuzi, au
Wapemba,” alisema.
Alisema ukurasa wa kwanza wa Rasimu ya Katiba unaeleza kuwa toleo
hili la Rasimu ya Katiba lilichapishwa katika Gazeti la Serikali kwa
mujibu wa Kifungu cha 20(2) ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya
83.
Alisema hiyo ni rasimu ya Tume ya Rais na si rasimu ya Wapemba.
Hata hivyo, alisema mjadala unaoendelea bungeni umekuwa na utaratibu
wa ubaguzi... “Watu wamebaguliwa humu na viongozi wakubwa wanapiga
makofi, Bunge hili limekuwa kama Bunge la Intarahamwe. Hii ni hatari kwa
nchi yetu. Wapemba, Waarabu, Wahindi, Wakongo,” alisema.
“Hii hatuhitaji, tunahitaji katiba ambayo itahakikisha kila mwananchi
anapata haki yake wote tuwe sawa bila kujali rangi zetu, jinsia zetu,
makabila yetu, huu ndiyo msingi aliotuachia Mwalimu Nyerere tuenzi
msingi huo.”
Alilalamikia kile alichokiita kuwa ni ubaguzi ndani ya Bunge na
kwamba kama Serikali haikutaka Katiba Mpya kwa nini imepeleka wabunge
Dodoma? Pia alihoji ni kwa nini ilitumia Sh70 bilioni katika Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
“Kwa nini mmetufikisha hapa? Jengo hili nimeambiwa limekarabatiwa kwa
Sh8.2 bilioni hali hamuamini Rasimu ya Katiba ama ilikuwa ni utaratibu
wa kupata hizo asilimia 10, ndiyo maana mmekarabati kwa gharama kubwa?”
alisema.
“Tunataka CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali),
akague matumizi ya fedha zilizotumika. Utatumiaje fedha nyingi wakati
hiyo katiba iliyowasilishwa kumbe huitaki kabisa.
“Hakuna utaratibu wowote wa kupiga kura na kufanya maamuzi kuhusu
sura hizi mbili. Tumechoka kusikiliza matusi. Tumechoka kudharau mawazo
ya wananchi, tumechoka ubaguzi, hatuwezi kuwa sehemu ya kundi
linalohamasisha ubaguzi ndani ya Tanzania hili hatukubali,” alisema.
No comments:
Post a Comment