Thursday, February 21, 2013

vitendo vya kikatili vyakithiri



UTAFITI wa Kitaifa wa Afya uliofanywa mwaka 2010 umeonyesha kuwa asilimia 72 ya wanawake na watoto wanaofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia Mkoa wa Dar es Salaam ikiwa nafasi ya pili kwa kuwa na asilimia 46 ambayo ni zaidi na kiwango cha ukatili huo nchi nzima ambacho ni asilimia 44.

Kwa mujibu wa utafiti huo ambao ulifanywa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii umeonyesha kuwa Mkoa wa Tanga una idadi ndogo ya vitendo hivyo ambapo ni sawa na asilimia 16.
Akizungumza jana Dar es Salaam katika mkutano uliohusisha viongozi wa Mkoa na Wilaya Dar es Salaam kuhusu mwongozo wa kisera na mwongozo wa kutoa huduma kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia, Mkuu wa Mkoa huo, Said Meck Sadick alisema vitendo hivyo vimekuwa vikiongezeka kila siku na kwamba vinatakiwa kukemewa.
Alisema kutokana na utafiti wa Kitaifa wa Afya uliofanywa mwaka 2010, hali ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto inaonekana kuwa mbaya hasa katika Mkoa wa Dar es Salaam jambo ambalo linatakiwa kuwekewa mikakati sahihi ili kutokomeza vitendo hivyo.

“Katika utafiti wa Kitaifa uliofanywa mwaka 2010, umeonyesha kuwa kiwango cha ukatili wa nyumbani kati ya wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49 ni asilimia 45 ambapo kwa Mkoa wa Dar es Salaam sababu kubwa inaweza kuwa mwingiliano wa watu kitu ambacho ni vyema kikaangaliwa kwa undani ili kuondoa vitendo hivyo,” alisema Sadick.

Alisema ukatili huo unajumuisha ukatili wa kimwili asilimia 25, kingono asilimia saba na asilimia 14 kwa aina zote mbili. Ukatili wa wanawake wajawazito ni asilimia tisa na asilimia 60 inaonyesha kwamba wanawake wajawazito hushurutishwa kufanya ngono na wapenzi wao bila ridhaa yao.
“Matukio ya ukatili wa kijinsia yanatofautiana kati ya mkoa na mkoa. Mkoa wa Dar es Salaam utafiti unaonyesha kuwa asilimia 46 ya wanawake na watoto wanafanyiwa vitendo hivyo na asilimia 74 katika Mkoa wa Mara,” alisema Sadick.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Usimamizi na Maendeleo ya Afya (MDH), Dk Guerino Chalamilla alisema kila mtu anatakiwa kuwa mstari wa mbele kukemea vitendo hivyo kwani havikubaliki katika jamii na kwamba ni kinyume na sheria.

Alisema MDH kwa kushirikina na Serikali wameweka mikakati sahihi ya kuhakikisha wanatoa elimu kwa watu wanaofanya vitendo hivyo ili kupunguza ukatili wa kijinsia wanaofanyiwa wanawake na watoto.
“Kwa kushirikina na Serikali tutahakikisha tunapiga vita na kuweka mikakati sahihi ambayo inasaidia kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake,” alisema Dk Chalamilla.     

No comments:

Post a Comment