Friday, April 12, 2013

Kerry aionya Korea ya Kaskazini

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, ameionya Korea ya Kaskazini kuwa itafanya kosa kubwa endapo itajaribu kombora lake la masafa ya kati. Akizungumza mjini Seoul nchini Korea ya Kusini hivi leo, Kerry amesema pia kuwa Korea ya Kaskazini haiwezi kamwe kukubaliwa kuwa taifa lenye nguvu za nyuklia, na kwamba Marekani itawalinda washirika wake barani Asia dhidi ya mashambulizi yoyote kutoka kwa utawala wa kibabe wa Kaskazini.

 Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani, amewaambia waandishi habari  kuwa, iwapo kiongozi wa Kaskazini, Kim Jong Un,ataamua kurusha kombora iwe ni kupitia bahari ya Japan au upande wowote ule, atakuwa ameamua kupuuza jumuiya nzima ya kimataifa na hivyo kuitenga zaidi nchi yake na ulimwengu.


Korea ya Kusini na Japan zimekuwa katika tahadhari ya hali ya juu baada ya kubainika kuwa huenda Kaskazini ikifanya majaribio ya makombora muda wowote baada ya kuhamisha makombora yake mawili hadi pwani ya mashariki. Nchi hiyo imeonya kuwa Japan ndiyo itakayolengwa kwanza iwapo kutatokea vita vya kinyuklia, baada ya Japan kutayarisha silaha za kujihami kukabiliana na makombora ya kinyuklia.Kerry anatarajiwa kuzuru Japan na China katika ziara yake inayokamilika Jumapili ambako atajaribu kuishawishi
China kuishinikiza Korea ya Kaskazini kusitisha mpango wake wa kinyuklia.



CHANZO DW

No comments:

Post a Comment