TCRA yatangaza kiama wanaokiuka sheria ya mawasiliano
Dar es Salaam. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kiama kwa watu watakaobanikia kuvunja Sheria ya Mawasiliano ya Electroniki na Posta (EPOCA) ya 2010, kwa kushindwa kutimiza vipengele vya sheria hiyo vinavyozuia matumizi na taratibu mbaya za uuzaji na usajili wa namba za simu za mkononi.
Licha ya onyo hilo, mamlaka hiyo imewakumbusha
wananchi baadhi ya makosa ambayo hufanyika katika taratibu za uuzaji,
utumiaji na usajili wa namba ili wajiepushe na rungu kali
litakalowakuta.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma kwenye
taarifa yake kwa umma jana, iliwataka wananchi kufahamu makosa ambayo
hukiuka vipengele vya sheria ya Epoca 2010 katika matumizi na biashara
ya namba za simu za mkononi.
Baadhi ya makosa yaliorodheshwa, ni kuuza au
kusambaza namba ya simu bila kibali cha mtoa huduma za simu ambaye ana
leseni kutoka TCRA; kutumia namba ya simu ambayo haikusajiliwa na kutoa
taarifa ya uongo au maelezo yasiyo sahihi wakati wa usajili.
Mengine ni kuchakachua simu ya mkononi au namba na kutoandikisha taarifa zake husika kabla ya kuitoa au kuiuza.
Profesa Nkoma aliwakumbusha watoa huduma wote na
wakala wao kuhakikisha wanazingatia kuweka kumbukumbu na taarifa kuhusu
wakala wao na kuandikisha watumiaji wanaonunua, au kupatiwa namba za
simu.
“Kutotoa taarifa za wateja bila idhini ya mamlaka
husika na wauzaji wote waliodhinishwa wana wajibu,” alisema Profesa
Nkoma.
No comments:
Post a Comment