Monday, June 3, 2013

UZINDUZI RASIMU YA KATIBA MPYA

Makamu wa Rais Dokta Mohamed Gharib Bilal amezindua rasimu ya Katiba mpya inayopendekeza kutovunjika kwa muungano na kuwepo na serikali tatu ambazo ni Serikali ya Shirikisho, Tanzania Bara na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mengine yaliyopendekezwa kwenye rasimu hiyo ni Spika wa Bunge na Naibu Spika wasitokane na wabunge na kwamba wasiwe viongozi wa Vyama vya Siasa.

Ni katika uzinduzi wa Rasimu ya Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndipo Mwenyekiti wa Tume ya Mchakato wa Katiba Mpya Jaji Mstaafu Joseph Warioba anabainisha mapendekezo ya Tume hiyo yaliyotokana na maoni ya wananchi kuhusiana na suala la muungano.

Mapendekezo mengine katika rasimu hiyo ni kutokuwepo na Viti maalumu na ukomo wa ubunge kwa awamu tatu huku wananchi wakipewa fursa ya kumuondoa madarakani mbunge aliyechaguliwa iwapo hawataridhika na utendaji wake.

Suala la mgombea binafsi limependekezwa katika rasimu hiyo kuanzia ngazi ya Kitongoji hadi Urais na Baraza la mawaziri lisitokane na wabunge waliochaguliwa na wananchi.

Akizindua Rasimu hiyo Makamu wa Rais Dk. Mohamed Gharib Bilal amewataka watanzania kutokuwa na jazba na badala yake kupitia rasimu hiyo kikamilifu na kutoa mapendekezo yatakayosaidia upatikanaji wa katiba yenye kukidhi mahitaji ya watanzania.

Zitto Kabwe ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Angela Kairuki ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria wanazungumziaje rasimu hiyo?


Rasimu hiyo imependekeza Tume ya Uchaguzi ibadilishwe na kuwa Tume huru ya Uchaguzi na kwamba majukumu yake yaunganishwe na Msajili wa Vyama vya siasa na mgombea wa urais atakayeshindwa ana haki ya kuhoji matokeo kwa Tume iliyomtangaza Rais ndani ya mwezi mmoja na kupatiwa ufumbuzi.

No comments:

Post a Comment