Saturday, July 20, 2013

VIONGOZI WA CUF WAJITOKEZA HADHARANI KUONYESHA NAMNA WALIVYOTEZWA NA JWTZ KATIKA SAKATA LA GESI MTWARA



VIONGOZI WA CUF WAJITOKEZA HADHARANI KUONYESHA NAMNA WALIVYOTEZWA NA JWTZ KATIKA SAKATA LA GESI MTWARA.
http://pamelamollel.files.wordpress.com/2013/06/cuf.jpg

WANACHAMA WATANO WA CUF WALIOTESWA NA ASKARI WA JWTZ WATOA USHUHUDA WAO.

Naibu Mkurugenzi Uchaguzi na Mipango wa CUF,  Shaweji Mketo akifafanua jambo kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu kuteswa kwa wanachama watano wa chama hicho na askari wa JWTZ mkoani Mtwara.
 Baadhi ya Viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kutoka (kulia) ni, Mwenyekiti wa Vijana Wilaya ya Mtwara Mjini, Ismaili Njalu.  Katibu wa Wilaya ya Mtwara mjini, Said Kulanga na Mwenyekiti wa Wilaya ya Mtwara mjini, Salum Mohamed wakiwaonesha waandishi wa habari majeraha waliyoyapata baada ya kupigwa na Wanajeshi wa  Wananchi  (JWTZ) katika mkutano uliofanyika Makao Makuu ya Chama hicho Dar es Salaam
VIONGOZI wa Chama cha Wananchi (CUF), wamejitokeza hadharani na kuonyesha namna ambavyo wamejeruhiwa vibaya kutokana na kipigo wanachodai kupigwa na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kutoka kikosi cha Naliendele mkoani Mtwara.

Viongozi hao, bila kujali jambo lolote, jana walilazimika kuvua mashati yao mbele ya waandishi wa habari makao makuu ya CUF Buguruni mjini Dar es Salaam na kuony

esha namna walivyojeruhiwa vibaya mgongoni.

Viongozi waliokumbana na kipigo hicho ni Naibu Mkurugenzi wa Oganizesheni, Uchunguzi na Bunge, Shaweji Mketo, Mwenyekiti wa Vijana Wilaya ya Mtwara Mjini, Ismail Njaro, Mwenyekiti wa Wilaya Mtwara Mjini, Salumu Mohamed.
Wengine ni Katibu wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Said Kuluga, dereva wao, Kashindye Kalungw

ana, Mkurugenzi wa Kikundi cha Ulinzi wa chama ‘Blue Guard’, Yassin Mjaliwa na Ismail Jamal ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho Mtwara Vijijini.

Viongozi hao, walishikiliwa na polisi mkoani Mtwara kwa siku 20, kwa tuhuma za kufanya kusanyiko haramu, uchochezi kati ya umma na Serikali pamoja na kuwa na kusudio la kufanya kosa la kuleta hofu kwa wananchi.

Migongo ya viongozi hao, ilionekana kuwa na majeraha mengi kuanzia kwenye mabega hadi sehemu za kiunoni, huku sura halisi ya miili yao ikionekana kama njia ya reli.

Alama za majeraha zilisababisha baadhi ya wanachama wa chama hicho waliokuwapo kwenye ukumbi wa mikutano, kuangua vilio.

Vilio vya wanachama hao, vilitokea baada ya viongozi hao kuvua nguo mbele ya waandishi huku wakiwaelezea kwa machungu jinsi walivyoteswa na askari wa JWTZ katika kambi ya Naliendele kabla ya kupelekwa polisi.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake, Mketo alisema hajawahi kupigwa na kunyanyaswa tangu kuzaliwa kwake na anaamini kipigo hicho ni mwanzo wa ukombozi wake na wananchi wa kusini.

Alisema akiwa na viongozi wenzake, walizingirwa na askari wa JWTZ eneo la njia panda ya Mtwara na Newala na kuanza kupigwa kisha kuingizwa kwenye gari lao na kupelekwa kambi ya Naliendele.

“Walianza kwangu na kuninyofoa kwenye gari na wakati huo kuna kanali mmoja aliingiza mkono mfukoni na kukuta Sh 85,000 nilizokuwa nazo, nilimshika mkono ndipo askari wengine waliponisogelea na kunihoji unamzuiaje bosi.

“Tulipofikishwa kambini tuliendelea kupigwa kwa kutumia fimbo na moja ya swali walilokuwa wakitutaka kusema, ni nani kiongozi wa Serikali anayetufadhili kwa lengo la kushawishi wananchi kupinga gesi isiondoke.

“Tulipozidi kukataa waliwaita vijana wao maarufu kama panaldo, ambao walitutaka kuvua nguo na kukumbatia mti na kuanza kutupiga na kutuhoji swali lile lile.

“Ilifika mahali nikazimia kwa zaidi ya saa nane, huku wengine wakiwa hoi, lakini walipokuwa wakiona tumezidiwa walitumwagia maji ya baridi yaliyokuwa na pilipili.

“Kwa kweli tuliteswa na hata chakula tulikuwa tunapewa cha baridi, binafsi ilifikia wakati nikawekewa dripu za maji na nilipozinduka nilichomoa chupa zile kwa sababu nilikuwa tayari kufa,” alisema.

Alisema Katibu wa CUF Mkoa wa Mtwara, Kaluga walimlazimisha kunyoa ndevu kwa kutumia kucha, jambo ambalo lilimsababishia maumivu makali.

Alisema pamoja na adhabu zote, askari wa JWTZ kambi ya Naliendele walimnyang’anya kompyuta yake ndogo (laptop), simu na daftari lililokuwa na taarifa za vikao.

Mketo alisema, CUF inaendelea kuwasiliana na wanasheria ili kufungua mashtaka dhidi ya JWTZ kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Naye, Mbunge wa Lindi Mjini, Baruan Salum (CUF), alisema kinachofanyika mkoani Mtwara ni dalili tosha taifa linaelekea pabaya.

“Hapa ninachokiona ni vyombo vya dola kutumika vibaya kwa kuwalinda viongozi wa Serikali na CCM, hawa askari wanapewa maagizo na wakubwa wao,” alisema Salum.

LIPUMBA NA JK

Katika hatua nyingine, Rais Jakaya Kikwete jana alikutana na Mwenyekiti CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ambako walijadiliana masuala mbalimbali ya uchumi wa nchi.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilisema viongozi hao walizungumzia mambo mbalimbali ambayo yatasaidia namna ya kuendelea kushirikiana kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.

“Jana Rais Kikwete, alikutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba.

“Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, viongozi hao wawili wamezungumzia masuala ya kitaifa na jinsi gani wadau mbalimbali wanavyoweza kuendelea kushirikiana kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Tanzania,” ilieleza taarifa hiyo.

CHANZOhttp://rweyemamuinfo.blogspot.com/

No comments:

Post a Comment