SUMAYE AKATA RUFAA KAMATI KUU CCM
Dodoma. Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye amekata rufaa Kamati Kuu
ya CCM kupinga adhabu ya onyo kali aliyopewa na chama kutokana na madai
ya kuanza kampeni za urais mapema kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Akizungumza na gazeti hili mjini Dodoma jana, Sumaye alisema kwa
ufupi hakuridhishwa na adhabu hiyo na kuthibitisha hilo, tayari amekata
rufaa.
Hata hivyo, alisema hadi jana hakuwa amepata mrejesho wowote kwa
sababu kanuni hazielezi ni muda gani anatakiwa kuwa amepewa taarifa
kuhusu rufaa hiyo.
Sumaye na wanachama wenzake, Edward Lowassa, Bernard Membe, Stephen
Wassira, William Ngeleja na January Makamba walitiwa hatiani kwa kuanza
kampeni mapema, hivyo kupewa onyo linalokwenda sambamba na kutowania
nafasi yoyote ndani ya chama kwa miezi 12.
“Siwezi kuwazungumzia wenzangu, nazungumza kwa upande wangu,
sikuridhishwa na adhabu hii na nimeshakata rufaa ingawa sijapata majibu
yoyote, naendelea kusubiri,” alieleza Sumaye.
Waziri Sumaye alikataa kuzungumzia hali ya utekelezaji wa adhabu
hiyo, akisema anachosubiri ni mwitiko wa rufaa yake aliyoiwasilisha
Kamati Kuu ya CCM, mwanzoni mwa mwezi huu. “Sina kumbukumbu nzuri
ilikuwa tarehe ngapi, lakini ni mwezi huu wa tatu.”
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa juu ya
rufaa hiyo alisema hana taarifa zaidi ya habari hizo kuzisikia kutoka
kwa mwandishi.
Hata alipotakiwa kueleza nani anatakiwa kuwa na taarifa hizo,
alisema: “Mimi ndiye msemaji wa chama, hakuna wa kuzungumzia suala hili
zaidi yangu. Kwanza inatakiwa ijulikane, rufaa hiyo imepelekwa ngazi
gani ya uongozi kwa sababu kila ngazi ina muda tofauti wa kufanya vikao
vyake vya uamuzi.”
Nnauye baada ya kuelezwa kuwa rufaa ya Sumaye imewasilishwa Kamati
Kuu ya CCM, alisisitiza kuwa hana taarifa nayo na kwamba haiwezekani
rufaa ipelekwe kwenye kikao kilichotoa adhabu husika.
Hata hivyo, Sumaye alisisitiza kuwa rufaa yake ameiwasilisha Kamati Kuu kwa mujibu wa kanuni zinazohusika.
Chanzo; mwananchi
No comments:
Post a Comment