MHE. SHY-ROSE BHANJI AKANUSHA HABARI ZILIZO ZAGAA MTANDAONI NA KUDAI NI MBINU ZA KUMCHAFUA.
Mimi Shy-Rose Bhanji, Mbunge wa Afrika Mashariki-Tanzania, ninapinga
vikali na kwa nguvu zote shutuma zilizotolewa dhidi yangu kupitia
mitandao mbalimbali ya kijamii.
Shutuma hizi hazina ukweli wowote na zinalenga, si kuniharibia, bali
kuchafua sifa yangu na utendaji kazi wangu katika Bunge la Afrika
Mashariki.
Lengo kuu la shutuma hizo ni kunivunja nguvu na ari ya kutetea maslahi
ya nchi yangu na Watanzania wenzangu kwani daima nimekuwa kikwazo na
mwiba kwenye ajenda zinazokiuka maslahi ya Tanzania.
Kwa mfano ardhi ya Tanzania kugawiwa kwa wana Jumuiya ya Afrika
Mashariki ni kinyume na Sera ya Tanzania. Nimekuwa miongoni mwa wabunge
wa Tanzania tulio mbele katika kulipinga suala hilo. Sishangai
likinijengea uadui.
Isitoshe, kwenye ajenda ya kumuondoa madarakani Spika wa EALA, Dk.
Margaret Zziwa, nilisimama kidete kwa kutounga mkono kwa sababu halikuwa
na maslahi ya Tanzania na yalikuwa kinyume na malengo ya ushirikiano wa
Jumuiya nzima.
Hoja ya kumuondoa Spika ilikuwa ni sehemu ya ‘mchezo mchafu’ ya ajenda
ya siri ya kumweka kwenye nafasi hiyo mjumbe mwingine kwa maslahi ya
wachache.
Jaribio hili la kumuondoka Spika lilifanywa na kushindikana mara tatu
baada ya kukosa sahihi za kutosha kutoka Tanzania, ikiwamo ya kwangu.
Baada ya kampeni ya kumwondoa Spika kushindwa, wabunge kadhaa walikuwa
wanasusia vikao vya Bunge wakati wameshachukua posho za vikao. Kwa mfano
kikao kilichofanyika hivi karibuni hapa Dar es Salaam.
Malumbano ndio yamekuwa yakitawala na kuinyima Bunge akidi ya kuendelea
na ajenda za mtangamano. Huu ni usaliti wa wazi kwa nchi zilizowachagua
na kuwatuma katika Bunge la EALA.
Ukijaribu kuwaasa kwamba mwenendo huo si sahihi, unageuka kuwa adui.
Na sasa wameamua kunitukana na kuzusha tuhuma kadhaa kupitia mitandao ya
kijamii ambako yote ni utunzi wa kisanii usiokuwa na chembe ya ukweli,
uhalali wala ushahidi.
Wahenga walisema ‘akutukanaye hakuchagulii tusi’. Walete ushahidi wa tuhuma zote dhidi yangu.
Kwa mfano, shutuma kwamba nililewa pombe ndani ya ndege, kuvunja chupa,
kufanya fujo na kufungwa pingu wakati wa safari ya Ubelgiji si kweli
hata kidogo.
Kama hizi tuhuma ni za kweli, kwanini hazikupelekwa polisi, serikalini au vyombo vingine vya sheria baada tu ya tukio?
Ijewe wamesubiri wiki mbili baada ya madai hayo ya tukio la kutunga
ndipo wajitokeze wakati wa kikao kinachoendelea mjini Kigali, Rwanda?
Kwanini wasubiri kikao cha Kigali ndipo uzushi huu utolewe?
Tuhuma kwamba nimewatukana marais wa nchi tatu hazina mashiko isipokuwa
kuhalalisha kampeni ya wale wanaonichafua na kuibua chuki kwa maraisi na
raia katika nchi za Kenya, Rwanda na Burundi.
Ninayo heshima kubwa sana kwa marais wa nchi zote tano na raia wa nchi
wanachama ambako mara zote nimepokewa na kuishi kwa amani na upendo
katika nchi hizo. Naahidi kuedeleza heshima hii.
Hainiingii kichwani ni wapi nilipoteza heshima hii isipokuwa kwa wale
wasionitakia mema ambao wamekusudia kufanikisha ajenda zao.
Shutuma zote dhidi yangu zimetengenezwa na watu ambao hatushabihiani katika hoja zetu na sishangai kwa hilo.
Mimi ni Mtanzania na ni Mbunge wa Tanzania. Hivyo nina wajibu wa kulinda
na kutetea maslahi ya Watanzania ili kuleta mtangamano wenye uwiano
sawa kwa nchi zote wanachama.
Ninaahidi nitaendelea kuwatumikia Watanzania kwa nguvu zangu zote na
kutoa ushirikiano kwa wabunge wengine wa EALA kwa manufaa ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
Nimeyasema haya nikiamini kuwa: “Uongo ukiachwa usemwe mara nyingi unaweza kuaminiwa kuwa ni ukweli.”
Umoja Wetu Ni Nguzo Yetu
Mungu ibariki Afrika Mashariki
Asanteni,
Shy-Rose Bhanji
Mbunge EALA
No comments:
Post a Comment