Leo ACT Wazalendo inatimiza mwezi wa tatu tangu mkutano mkuu wa kuchagua viongozi wake wa kitaifa ambapo baadhi yetu tumechaguliwa kuongoza chama chetu. Katika kipindi hicho tumeweza kutambulisha chama chetu katika makao makuu ya mikoa 22 ya Tanzania bara. Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro tumefikia wilaya zake na mkoa wa Dar Es Salaam tutaingia tarehe 4 Julai 2015. Baadaye tutakwenda kufanya mikutano katika miji ya Arusha na Moshi. Mikutano yetu imekuwa na mafanikio makubwa sana. Tunamshukuru mungu.
Leo tupo kibaha katika mkoa wa Pwani. Leo pia Mwenyekiti wetu yupo Karatu katika mkoa wa Arusha. Katika awamu hii ya ziara tumekuwa pia tukifafanua kuhusu Azimio la Tabora linalohuisha Azimio la Arusha. Katika Azimio la Tabora tumeamua kufanya kampeni kurejesha Miiko ya Viongozi. Sisi tunaamini kuwa Miiko ya Viongozi ambayo inadhibiti viongozi wa umma kujilimbikizia Mali ndio mwarobaini dhidi ya ufisadi nchini mwetu.
Nilipokuwa Nachingwea juzi nilitoa mfano wa wanasiasa 4 wa chama cha CCM ambao niliwataka kutoa ufafanuzi kuhusu masuala yanayozungumzwa dhidi yao. Hii ilikuwa katika kuonyesha umuhimu wa Miiko katika aina Mpya ya siasa tunazotaka kuanzisha katika nchi yetu. Bado narudia kutoa wito kwa wagombea wote wa Urais kutoka vyama vyote kuacha porojo za kupambana na ufisadi na badala yake waseme namna watakavyopambana. Sisi tunaamini kuwa njia pekee ya uhakika ya kupambana na ufisadi ni kurejesha Miiko ya Viongozi.
Nataka kuwahakikishia wataanzania kuwa chama chetu kitaweka mgombea Urais mwaka huu na tutashinda. Mimi siamini hata kidogo kuwa mabadiliko yataletwa kupitia CCM na ndio maana siku zote nimekuwa nikiwasihi wanasiasa wenzangu vijana wanaotaka kuongoza nchi yetu kama January Makamba na Mwigulu Nchemba waondoke CCM waje kwenye chama hiki ili kujenga Tanzania Mpya yenye misingi imara.
Chama chetu kinataka kujenga siasa Mpya zenye lengo la kurejesha nchi kwenye misingi. Kwa namna ambavyo ufisadi umetamalaki nchini kwetu, kurejesha Miiko ya viongozi hakuepukiki. Ninaamini wanasiasa vijana wana uwezo huo kwani bado hawajaingia kwenye tabia hii mbaya ya kujilimbikizia Mali.
Tunawataka Watanzania kuwashinikiza wanasiasa kutangaza Mali na Madeni yao ikiwemo maslahi mbalimbali kabla ya kushika nyadhifa za uongozi wa umma. Ninawataka vijana wa Tanzania kuungana nasi katika kufanya mabadiliko makubwa kwenye nchi yetu ili kujenga uchumi unaozalisha ajira na kuondoa umasikini, kuboresha huduma za jamii kama Maji, Afya na Elimu, kupambana na ufisadi na kuziba nyufa za udini na ukabila kwa kurejesha ujamaa.
Wananchi wa Kibaha, mkoa wenu wa Pwani ni moja ya mikoa masikini kabisa nchini mwetu. Ni mkoa ambao hata juhudi za awali za kujenga viwanda ili kuukomboa zimezimwa kwa kubinafsisha viwanda vilivyokuwa hapa Kibaha. ACT Wazalendo inataka kushirikiana nanyi kujenga heshima ya mkoa wa Pwani.
Tutarejesha viwanda ili kutoa ajira kwa vijana wetu. Pwani yaweza kutumika kupunguza msongamano jijini Dar Es salaam kwa kujenga container depots kibaha na chalinze na hivyo kuongeza ajira kwa vijana wetu.
Wananchi wa mkoa wa Pwani tumekuja kutambulisha chama chetu kwenu. Tunaomba mtuunge Mkono. Nawashukuru sana
Zitto Kabwe
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo
No comments:
Post a Comment