MBOWE AMTAKA KIKWETE ASIKUBALI VITISHO.
![]() |
Mwenyekiti wa Chadema,Freeman Mbowe akihutubia moja ya mikutano ya kukimarisha chama hivi karibuni mkoani Arusha. |
Arusha
MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amemtaka Rais Jakaya
Kikwete kutokubali vitisho vinavyotolewa na baadhi ya wabunge wa CCM,
kwamba wako tayari Bunge livunjwe kuliko kupitisha mabadiliko ya Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba.
Mbowe alisema kuwa hakuna mwenye ubavu
wa kurudi kwenye uchaguzi endapo Bunge litavunjwa, huku akiweka bayana
kuwa mkutano wa Bunge ujao utakuwa na patashika endapo wabunge wa CCM
watataka sheria ya mabadiliko ya katiba iendelee kubaki na kasoro bila
kufanyiwa marekebisho ya msingi.
Angalizo hilo alilitoa jana jijini
hapa wakati akifungua mkutano wa Baraza la Uongozi la CHADEMA Kanda ya
Kaskazini, inayojumuisha mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara
na kuhudhuriwa na muasisi wa chama hicho, Edwin Mtei.
Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai,
alisema wakati wa mazunguzo kati ya Rais Kikwete na viongozi wa vyama
vya siasa, aliwataka wasitishe uamuzi wa kuingiza wananchi barabarani
kufanya maandamano.
Alisema kuwa walimweleza rais kuwa hawapendi kufanya maandamano ila inabidi pale mambo yanapokuwa hayaendi sawa.
"Jumatatu tutakuwa na kikao cha Kamati
ya Bunge ya Uongozi ambayo mimi pia ni mjumbe wake, hivyo kikao hicho
kitaniwezesha kujua ni mambo gani yaliyo kwenye sheria ya mabadiliko ya
katiba yatakayorudishwa bungeni kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho.
"Nimtake Rais Kikwete asikubali
kutishwa na wabunge na mawaziri aliowateua mwenyewe, kwanza hakuna
mbunge wa CCM mwenye ubavu wa kurudi kwenye uchaguzi kama rais atavunja
Bunge. Nashangaa rais anatishwaje na watu aliowaajiri yeye?" alihoji.
Alisema CHADEMA wanaenda bungeni kwa
roho safi ila kikao hicho kitakuwa na patashika endapo maslahi ya taifa
yatawekwa kando na kutangulizwa ushabiki unaoendeshwa na baadhi ya
wabunge wa CCM.
Mbowe alisema katiba ni mali ya
Watanzania wote, huku akiweka wazi kuwa kwa sasa kuna hofu miongoni mwa
wananchi kwani hawajui uchaguzi mkuu ujao utafanyika chini ya katiba
ipi.
Alifafanua kuwa chama chake kitakuwa
kimekamilisha mchakato mzima wa kukiendesha kupitia mfumo wa dijitali
ifikapo mwisho wa mwaka huu.
Kwama wanatarajia taarifa zote,
mawasiliano baina ya viongozi na wanachama pamoja na uwekaji wa
kumbukumbu utafanyika kwa kupitia mfumo wa mawasiliano wa dijitali.
Naye Mtei alisema kuwa anapata faraja
kuona namna chama hicho kinavyokubalika kwa wananchi jambo linaloufanya
moyo wake kudunda akiamini kwenye uchaguzi mkuu ujao kitapata ridhaa ya
wananchi kuongoza dola.
No comments:
Post a Comment