TBL Yazindua mashindano ya mitindo na ubunifu nchini
Meneja masoko wa TBL Fimbo
Butallah akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam kwenye
uzinduzi wa mashindano ya ubunifu na mitindo kwa wanafunzi wa vyuo vya
elimu ya juu nchini ( Redd's Uni-Fashion Bash 2013) yatakayofanyika
katika mikoa ya Dar Es Salaam,Mwanza,Iringa na Kilimanjaro.Kushoto ni
Meneja mawasiliano na habari wa Tbl Edith Mushi.
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL)
kupitia kinywaji chake cha Redd’s Original imezindua tamasha la mitindo
na ubunifu kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu hapa nchini,
litakalojulikana kama ‘Redd’s Uni-Fashion Bash’.
Akizungumza katika uzinduzi huo
uliofanyika Dar es Salaam jana, Meneja Masoko wa TBL, Fimbo Butallah
alisema, tamasha hilo lenye lengo la kuinua vipaji vya wanafunzi katika
tasnia ya mitindo, linatarajiwa kuanza mwezi huu na kumalizika mwezi
ujao.
Butallah alisema, tamasha hilo kwa
sasa litashirikisha vyuo vyote vya elimu ya juu vilivyopo katika Mikoa
ya Dar es Salaam, Iringa, Kilimanjaro na Mwanza.
“Tunataka kuinua vipaji vya
wanafunzi wa vyuo katika tasnia ya mitindo, kupitia maonyesho
yakatakayofanywa na wanafunzi wa vyuo hivyo, hapa tunataka wale wenye
ubunifu kuonyesha ubunifu wao wa mitindo, hivyo hii ni fursa kwao
kujitangaza na kudhihirisha uwezo wao,” alisema Butallah.
Kuhusu ushiriki, Butallah alisema,
kutakuwa na fomu maalumu zitakazosambazwa katika vyuo husika, ambapo
wanafunzi wanamitindo na wabunifu watazijaza na majaji watazipitia na
kupata wabunifu 10 na wanamitindo wa idadi hiyo kutoka kila mkoa, ambao
watapata fursa ya kuonesha mavazi yao siku ya tamasha.
Kuhusu zawadi, Meneja Habari na
Mawasiliano wa TBL, Edith Mushi alisema, kutakuwa na zawadi mbalimbali
kutoka Redd’s Original, ambapo washindi watano wa ubunifu na idadi kama
hiyo ya wanamitindo kutoka kila mkoa watajiondokea na fedha taslimu.
Edith alisema, kwa upande wa
wabunifu mshindi wa kwanza ataondoka na Sh 700,000 wa pili Sh 500,000
watatu Sh 300,000 huku wa nne na watano kila mmoja akiondoka na Sh
100,000.
Kwa upande wa wanamitindo mshindi
wa kwanza atajiondokea na Sh 500,000 wa pili Sh 400,000 wa tatu Sh
300,000 wakati wanne na watano wakipata Sh 100,000 kila mmoja.
“Tuna imani kubwa zawadi hizi
zitaongeza chachu kwa wabunifu na wanamitindo kuendeleza fani hii ya
mitindo. Lakini matamasha haya pia yatahusisha burudani za aina
mbalimbali za kuvutia.
“Hii itakuwa sehemu muhimu ya
kuwakutanisha wanafunzi wa vyuo na kada mbalimbali katika kufurahia na
kubadilishana mawazo juu ya masuala ya ubunifu na mitindo, kwani
kinywaji cha Redd’s Original kimekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza
tasnia ya urembo, ubunifu na mitindo hapa nchini,” alisema Edith.
Kinywaji cha Redd’s Original pia
ndicho kinachodhamini shindano la Redd’s Miss Tanzania na kinazalishwa
na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
No comments:
Post a Comment