KITENDO cha kuwavua uongozi aliyekuwa
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati
Kuu, Dk Kitila Mkumbo, kimesababisha ziara ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willibrod Slaa mkoani Kigoma, iahirishwe.
Hatua hiyo imefikiwa na uongozi wa
Chadema Mkoa, baada ya kupata taarifa za mipango haramu ya kusababisha
uvunjifu wa amani wakati kiongozi huyo atakapokuwa mkoani Kigoma.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Kigoma, Jafari Kasisiko, alisema hayo jana
katika mkutano wake na waandishi wa habari, alipokuwa akizungumzia
kusitishwa kwa ziara hiyo.
Kasisiko alisema wameandika barua kwenda
Makao Makuu ya Chadema jijini Dar es Salaam, kuomba kuahirishwa kwa
ziara hiyo ya Dk Slaa kwa kile ambacho uongozi wa Mkoa unaona hauna
uwezo wa kudhibiti hali hiyo, iwapo itatokea.
Kabla ya kuomba kuahirishwa kwa ziara
hiyo, Mwenyekiti huyo alisema Baraza la Ushauri la Mkoa Kigoma, lilikaa
na kupokea taarifa kutoka kwa viongozi wa majimbo mbalimbali ya mkoa,
zilizoonesha wapenzi wengi wa Chadema katika maeneo hayo, hawako tayari
kumpokea Dk Slaa.
Alisema viongozi wengi waliohudhuria
kikao hicho cha ushauri, walieleza kuwa maeneo yao kwa sasa hawako
salama kumpokea kiongozi huyo wa kitaifa, kutokana na kuendelea kwa
vitendo vya baadhi ya wanachama kuchoma bendera na kuharibu matawi ya
chama hicho.
Alitoa mfano wa Jimbo la Kigoma
Kaskazini, ambako vurugu ni kubwa zaidi na taarifa zilizopatikana
zinaeleza kuwa iwapo Dk Slaa atafika maeneo hayo, wanachama na baadhi ya
wapenzi wa chama hicho, wamepania kumfanyia vurugu mbalimbali, ambazo
mwisho wake siyo mzuri kwa chama hicho.
Pamoja na hali hiyo, Mwenyekiti huyo wa
Chadema Mkoa Kigoma, alisema ziara hiyo ya Katibu Mkuu haina uhusiano
wowote na hatua ya Kamati Kuu ya Chadema kumvua uongozi Naibu Katibu
Mkuu huyo, na kwamba viongozi wa chama hicho mkoani humo wanaunga mkono
hatua iliyochukuliwa na Kamati Kuu.
Katibu Mkuu wa Chadema alitarajiwa
kuanza ziara ya kuimarisha chama mkoani Kigoma Desemba 5 mwaka huu,
ambapo alitarajiwa kuzunguka majimbo yote ya uchaguzi mkoani Kigoma na
kuhitimisha ziara hiyo Desemba 13 mwaka huu.
Gazeti hili lilitafuta viongozi wa
Chadema makao makuu, ambapo simu zao zilikosekana. Baadaye mmoja wa
maofisa aliyekuwa mstari wa mbele kutoa taarifa kuhusu yanayojiri baada
ya ya akina Zitto kung’olewa madaraka, alisema maandalizi ya ziara hiyo
yanaendelea.
"Leo ndiyo mmepiga simu ili kufanya
uwiano, siku zote mnaandika habari za umbeya, hamjawahi kupiga simu. Leo
imekuwaje?," alisema ofisa huyo, ambaye alikuwa mstari wa mbele kutoa
namba za wasemaji wa kutetea hatua ya Kamati Kuu.
"Kwa taarifa yako sasa, tayari huko
Kigoma watu wanafanya maandalizi makubwa ya kumpokea Katibu Mkuu Dk
Willibrod Slaa, wewe unafikiri huo ni uamuzi wa mtu mmoja tu, hiyo ni
lazima vikao vikae ndiyo viahirishwe. "Mpaka sasa ninapoongea na wewe
hapa, maandalizi ni makubwa sana, naomba usininukuu mimi. Nakutumia
namba za watu ambao watakupa habari kamili ambao wapo huko Kigoma,"
alisema na baadae kutoa namba hiyo.
Hata hivyo, baadae namba hiyo ilipotolewa, haikupatikana.
chanzohttp://habarileo.co.tz/
No comments:
Post a Comment