Tuesday, March 5, 2013

AFISA HABARI WA YANGA EZEKIELI KAMWAGA

Licha ya Simba kuchapwa 4-0 katika mechi yao ya ugenini ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Recreativo de Libolo ya Angola na hivyo kufungishwa virago juzi kwa kipigo kibaya cha jumla ya mabao 5-0, wachezaji wa klabu hiyo ya Msimbazi hawakutaka kulala na badala yake waliendelea kama kawaida na ratiba yao ya mazoezi wakiwa nchini humo kujiandaa kwa mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara watakayocheza Jumapili dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

Afisa habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga, aliiambia NIPASHE jana kuwa wachezaji wao walifanya mazoezi jana asubuhi ili kujiweka 'fiti' kabla ya kucheza nyumbani dhidi ya 'Wagosi wa Kaya' kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba ambao ni mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Bara, wanakamata nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kufikisha pointi 31, sawa na wapinzani wao wa Jumapili (Coastal) ambao wanakamata nafasi ya nne kwa kuzidiwa tofauti ya magoli na 'Wanamsimbazi'.

Mahasimu wa jadi wa Simba, klabu ya Yanga, ndiwo wanaoongoza ligi hiyo wakiwa na pointi 42, pointi sita zaidi ya Azam wanaowafuatia katika nafasi ya pili. 

Akieleza zaidi, Kamwaga alisema kuwa baada ya mazoezi yao jana asubuhi,  timu yao ilianza safari ya kuelekea Luanda (mji mkuu wa Angola) na leo mchana inatarajiwa kuanza safari ya kurejea nchini na kutua jijini Dar es Salaam usiku.

Kipigo kikubwa cha mwisho Simba katika michuano ya Afrika kabla ya kung'olewa na Libolo kwa mabao 4-0 juzi kilikuwa mwaka 2009 wakati ilipofungwa 5-1 na Harass Al Hadoud ya Misri kwenye mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa iliyofanyika jijini Alexandria.

Katika hatua nyingine, imedaiwa kuwa hali si shwari ndani ya timu hiyo baada ya kuibuka kile kinachoelezwa kuwa ni makundi miongoni mwa baadhi ya viongozi hadi kwa wachezaji.

Akizungumza na gazeti hili jana, mmoja wa viongozi wa klabu hiyo alisema kwamba Simba imekuwa na tatizo la kutoshirikiana vyema na kutokuwa na maamuzi ya pamoja kuanzia kwa viongozi, wachezaji hadi kwa wanachama na jambo hilo lisiposhughulikiwa haraka linaweza kuwaathiri zaidi.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment