KANISA LAWATAKA WACHUNGAJI WAJIUZULU CHADEMA
Mwenyekiti wa
Chadema Kanda ya Kusini ambaye pia ni Mchungaji wa Kanisa la
Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Joseph Matare amejiuzulu
nafasi yake hiyo kutokana na kanisa lake kuwataka wachungaji wake ambao
ni viongozi wa vyama vya siasa kuachana na nafasi zao za kisiasa.
Joseph Matare akizungumza na waandishi wa habari mjini Songea amesema
kuwa ameamua kujiuzulu nafasi yake ya uongozi wa Chadema Kanda ya Kusini
inayojumuisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma baada ya kanisa lake
katika mkutano wake wa kanda kuagiza wachungaji wake ambao ni viongozi
wa siasa kuachia nafasi zao na badala yake wasimamie kazi ya Mungu
katika makanisa yao.
“Kufuatia maagizo ya mkutano huo wa kanisa uliofanyika Njombe nimeamua
kutii... nimeamua kujiuzulu na katibu wangu mkuu, Dk Willibrod Slaa
nilimjulisha tangu tarehe 4 Juni mwaka huu,” alisema Matare katika
taarifa yake ya kujiuzulu.
Amefafanua kuwa muda wa viongozi wa kanda ulikuwa ni wa muda na wa mpito
hadi uchaguzi wa kanda utakapopita ambao ulipaswa kufanyika Juni 2014
na kwamba muda umeongezwa hivyo ameona aheshimu maagizo yaliyomweka
madarakani.
Hata hivyo, Matare anasema kuwa anawatia moyo makamanda wote wa Chadema
waliobaki kuendelea kupigania nchi ili iondokane na uovu unaotendeka
sasa na kwamba Mungu atakuwa nao wale wote wanaotafuta haki kwa ajili ya
wananchi walio wengi.
No comments:
Post a Comment