Saturday, January 3, 2015

....................................................................................ALLIANCE FOR CHANGE AND TRANSPARENCY TANZANIA ACT-TANZANIA P.O.BOX 105043, Mob: +255 787 457 970, +255 0755 023 503, Dar Es Salaam Tanzania. Email: diplomatictable@gmail.com TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI. Ndugu wanahabari, Chama cha Alliance For Change and Transparency Tanzania (ACT-Tanzania), kinapenda kuwaatarifu wanachama wake wote kuwa wajiepushe na upotoshaji unaofanywa na baadhi ya waliokuwa wanachama wetu na waliokuwa viongozi wetu waliofukuzwa uanachama na kikao halali cha chama, tarehe 31 Desemba 2014. Wanachama na wananchi watambue kuwa chama chetu hakina wajumbe wa Kamati Kuu wala Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa kuwa ndiyo kwanza kinajiandaa kufanya uchaguzi wake. Uchaguzi mkuu wa ACT, unatarajiwa kufanyika Mei mwaka huu. Hivyo basi, kikao kinachoitishwa na mwaliko wake kutumwa na aliyekuwa Katibu Mkuu, Bw. Samson Mwigamba, ni batili kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi. Wanaokiitisha siyo wanachama wa ACT na hawana mamlaka ya kufanya kazi za chama chetu. Kamati iliyowaondoa katika nyadhifa zao na kuwavua uwanachama, ambayo ilikuwa chini ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama chetu, Bw. Lucas Kadavi Limbu na maamuzi yake kutangazwa kwenye vyombo vya habari, ndiyo chombo halali cha kuitisha mikutano na kujadili mambo ya chama kwa mujibu wa katiba na sheria Na. 5 ya Vyama vya Siasa nchini. Aidha, ACT-Tanzania kinamuonya Bw. Mwigamba na mshirika mwenzake, Prof. Kitila Mkumbo kuacha mara moja kupotosha umma juu ya katiba ya chama kwa kuwa hawana weledi wa kuchambua katiba na ndio sababu wanashindwa kufahamu tofauti kati ya mamlaka na majukumu; na kutumia jina la chama kwa maslahi binafsi. Katibu wa chama ni taasisi na wala sio Mwigamba kama wanavyotaka kuhalalisha kwamba bila yeye vikao haviwezi kuitishwa, ofsi ya katibu mkuu yenye majukumu na wajibu wa kuitisha vikao (kuhakikisha vikao vinaalikwa) na sio yenye mamlaka ya kualika au kutoalika kama wanavyopotosha. Tunawataka wasome vizuri katiba wajue na wapate tafasiri ya sentensi isemayo, Mwenyekiti ndiye kiongozi mkuu wa chama, hivyo wajipime kwanza na wampime mwanasheria wao kabla hawajachukua hatua zinazoweza kuharibu heshima yao zaidi, Bw. Mwigamba na Prof. Kitila, ni watu wakaidi mno, wabinafsi na waroho wakubwa wa madaraka. Kuwavumilia katika taasisi yoyote ile kunahitaji kuwa na moyo wa chuma; historia zao huko walikofukuzwa zinajulikana. Kikao kinachoitishwa wasemacho ni cha kamati kuu tarehe 05/01/2015 sio cha chama cha ACT-Tanzania, pengine ni kikao cha harusi ya rafiki yao. Nembo iliyotumika kualika kikao hicho cha Mwigamba sio nembo ya ACT-Tanzania. Vilevile, tunapenda kuufahamisha umma kuwa tulipata taarifa kwamba aliyekuwa Mwekahazina wetu ambaye alijiuzulu na kujiondoa kwenye chama, kabla ya kikao cha tarehe 31 Desemba 2014, Bwana Peter Mwambuja alifika katika ofsi za makao makuu na kuingia ndani ya ofsi kwa funguo zisizojulikana alizitoa wapi. Hali hiyo ilipelekea tufunge ofsi hizo kwa muda na chama kimepeleka taarifa kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), hivyo mtu yoyote atakayeingia katika ofisi hizo bila idhini ya uongozi halali wa chama, atahesabika kuwa mwizi na mvamizi. Ofisi za chama zitakuwa wazi mara baada ya viongozi kumaliza mikutano yao huko Zanzibar. ACT-Tanzania HAINA UBIA NA CUF Aidha chama kinatoa onyo kali kwa Wanachama na viongozi waliobeba mabango na kuvaa mavazi yenye jina la ACT-Tanzania kwenda Mtwara kuhudhuria mkutano wa CUF huku wakizomewa na kulazimishwa kushusha bendera za ACT-Tanzania walizokuwa nazo katika viwanja vya mashujaa na kusababisha mkanganyiko kwa wananchama na wananchi kuhusu kushirikiana kwa CUF na ACT-Tanzania . Chama cha ACT-Tanzania hakijawahi kukaa wala kujadili na CUF juu ya jambo la kushirikiana, lakini ni haki ya mwanachama wa chama chochote kuhudhuria mkutano wa chama kingine, ila ni kosa kuhamasisha na kuchangishana pesa na kukodi magari kwenda katika mikutano mikoa ya mbali kuhudhuria mkutano wa chama kingine ambako hata hawajahi kufanya zoezi hilo katika kueneza chama chao, Hali hiyo inaonyesha kuwa wana mapenzi ya dhati na chama hicho cha wananchi CUF na hawana mapenzi na ACT-Tanzania, hivyo waliozomewa hawakutumwa na chama bali ni mapenzi yao binafsi waliyoyaonyesha bila kuweka tahadhari ya mikanganyiko inayotafasiriwa kuwa ni muungano wa ACT-Tanzania na CUF. Mwisho chama kinawaomba wanachama wajitume katika kulitumikia taifa na kuwajibika katika zamu zao ili Taifa lisonge mbele. Asanteni sana,

No comments:

Post a Comment